• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakulima, wafugaji wataka usaidizi wa serikali

Wakulima, wafugaji wataka usaidizi wa serikali

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wengi walipata hasara ya mazao yao baada ya Covid-19 kuingia nchini.

Baadhi ya mazao hayo ni pamba, alizeti na Soya.

Mfanyabiashara wa Thika Bw Kihara Gathua alisema wakulima wengi wanapata hasara kutokana na hali ngumu waliopitia wakati huu wa janga la Covid-19.

Alisema kutokana na hali hiyo bei za mbegu za mazao hayo zitapanda maradufu hata wakulima wengi watashindwa kuendesha kilimo cha mazao hayo.

“Ni vyema serikali kufanya juhudi kuona ya kwamba wakulima kama hao wanasaidiwa ili waendelee kupanda mazao hayo,” alisema Bw Gathua.

Alisema chakula cha mifugo kwa wakati huu kinatolewa nchi za nje kama Malawi na Uganda kwa bei ya juu ambayo wafugaji wa kawaida hawawezi kugharimia.

“Kwa hivyo, Mwaka Mpya wa 2021 serikali inastahili kufanya juhudi kuona ya kwamba wakulima na wafugaji wanasaidiwa ili kujiendeleza,” alisema Bw Gathua mnamo Jumanne mjini Thika.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina ambaye yuko kwenye kamati ya mauzo katika bunge majuzi alisema bidhaa zinazotengenezwa hapa nyumbani hazifai kuingiza za aina sawa na hizo nchini.

Badala yake alipendekeza zitozwe ushuru maradufu ili “kuokoa bidhaa zetu za hapa nchini.”

“Watu wa juakali wanaendesha kazi nzuri ya kutambulika na kwa hivyo ni vyema bidhaa zao zitambulike na serikali ili nao wanufaike kiuchumi,” alisema mbunge huyo.

Alipendekeza bidhaa zinazoundiwa hapa nchini zithaminiwe na Wakenya na wahimizwe kuzinunua ili “kuinua uchumi wetu.”

“Ili kukuza uchumi wetu tutalazimika kuthamini bidhaa zetu za hapa nchini. Nchi kama China, Korea, na hata Japan zinahusudu bidhaa zao kuliko zile zinazotoka nchi za nje,” alisema kiongozi huyo.

Alipongeza juhudi zinazofanywa na baadhi ya viwanda vya hapa nchini kwa kuunda vifaa-kinga (PPE) vinavyotumika hospitalini wahudumu wa kujikinga wasipate maambukizi ya Covid-19.

“Hii ni njia moja ya kujitegemea kwa kuunda bidhaa zetu wenyewe bila kutegemea nchi za nje. Hapo awali serikali iliagiza bidhaa hizo kwa kutumia mamilioni ya fedha lakini sasa tunajitegemea kwa kiwango fulani,” alisema mbunge huyo.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Nakuru ilivyoukaribisha Mwaka Mpya 2021

Amerika yamshutumu Rais Museveni kunyanyasa Wine