Ruto alivyozima kabisa juhudi za Gideon Moi kutawala Rift Valley

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto ameanza juhudi za kumtenga kiongozi wa chama cha Kanu Gideon Moi katika siasa za Bonde la Ufa.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Naibu wa Rais kumvutia upande wake kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto ni pigo kubwa kwa Seneta wa Baringo Bw Moi.

Naibu wa Rais Ijumaa alimpokea rasmi gavana wa zamani wa Bomet Bw Ruto katika eneo la Sotik, ambapo aliongoza mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya wahudumu wa bodaboda na kisha kukabidhi basi kwa timu ya soka ya Silibwet FC.

Mwezi uliopita, kiongozi wa CCM Ruto alitangaza kuwa ataunga mkono Seneta Moi katika kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2022 baada ya kuhudhuria mkutano wa Kanu katika Kaunti ya Bomet.Baadaye alisema kuwa alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya kubanwa na Katibu Mkuu wa CCM Zedekiah Kiprob Buzeki.

Lakini wiki iliyopita, kinara wa CCM alibadilika na kusema kuwa yuko tayari kushirikiana na Naibu wa Rais Ruto kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Mimi sijaungana na yeyote. Kufikia sasa hakuna mtu ameniomba nimuunge mkono 2022 katika kinyang’anyiro cha urais. Naibu wa Rais akija kwangu na anisihi nimuunge mkono tutajadiliana. Akiafikiana na maono ya chama cha CCM, basi sitakuwa na budi kushirikiana naye,” akasema.

Mbali na gavana wa zamani, Naibu wa Rais Ruto Ijumaa alifanikiwa kuwatia kibindoni madiwani 22 wa chama cha CCM.Naibu wa Rais Ijumaa alisema kuwa atatumia chama cha United Democratic Alliance (UDA) endapo chama cha Jubilee kitamnyima tiketi ya kuwania urais 2022.

Hiyo inamaanisha kuwa huenda chama cha UDA kikafanya muungano na CCM au vitavunjiliwa mbali na kubuni chama kipya.Bw Isaac Ruto na Seneta Moi wamekuwa wakishirikiana kisiasa na mwaka jana walitia mkataba wa kuunda muungano na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Baada ya kutia saini mkataba huo, ilitarajiwa kwamba kiongozi wa CCM angepewa wadhifa serikalini lakini aliendelea kuachwa kwenye ‘baridi’.Inaonekana Naibu wa Rais aliamua kumwendea kiongozi wa CCM kutokana na hofu kwanga yeye na Bw Moi wangechangia kugawa kura za eneo la Bonde la Ufa katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Kwa upande mwingine, inaonekana gavana wa zamani aliamua kujiunga na Naibu wa Rais kwa lengo la kutaka kuwania tena ugavana wa Bomet baada ya kupoteza kiti hicho 2017 aliposhindwa na Joyce Laboso wa Jubilee,” anasema wakili Felix Otieno.

Isaac Ruto na Naibu wa Rais walianza kuwa maadui wa kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2013; hali iliyomlazimu kuunda chama chake cha CCM alichotumia kuwania ugavana 2017 lakini akabwagwa na Laboso aliyefariki Julai 2019.

Bw Ruto na Naibu wa Rais walikutana mara ya mwisho ana kwa ana hadharani mnamo 2018 katika eneo la Siongiroi, eneobunge la Chepalungu,Kaunti ya Bomet.Juhudi za kiongozi wa CCM kutaka kumng’oa Gavana wa Bomet Hillary Barchok kwa kutumia madiwani wake ziligonga mwamba.

Wiki iliyopita alifokewa vikali na vijana katika eneo la Kuresoi, Kaunti ya Nakuru. Vijana hao walimtaka kuungana na Naibu wa Rais ikiwa alihitaji kujinusuru kisiasa.

“Ingekuwa vigumu kwa Isaac Ruto kushinda kiti cha ugavana bila baraka za Naibu wa Rais. Kwa sasa Dkt Ruto ana usemi mkubwa sana katika eneo la Bonde la Ufa,” anasema Bw Otieno.

Hatua hiyo ya Bw Ruto inamaanisha kuwa ushawishi wa Seneta Gideon – ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta umesalia katika Kaunti ya Baringo pekee.Wiki mbili zilizopita, vijana wafuasi wa Naibu wa Rais walizuia Seneta Moi kwenda kutawazwa kuwa mzee wa jamii ya Talai.

Bw Moi aliyekuwa amendamana na viongozi wengine wa mrengo nwake alipata barabara za kuelekea katika maeneo ya Talai na Kapsisiywa zimefungwa na kundi la vijana.Hivi karibuni mwenyekiti wa Kanu Moi alifanikiwa kumpokonya Dkt Ruto wabunge William Chepkut (Ainabkoi) na Silas Tiren (Moiben) na gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos.

Mbunge wa Charangany Joshua Kutuny alikuwa upande wa Bw Moi lakini uhusiano wao umedorora katika siku za hivi karibuni.Lakini mbunge wa Kimilili Didmus Barasa aliambia Taifa Jumapili kuwa lengo kuu la Dkt Ruto ni kuhakikisha kuwa Seneta Moi anaachwa mpweke kufikia 2022.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa wakazi wa Bonde la Ufa pamoja na nchi nzima wanaungana na kuzungumza kwa sauti moja,” akasema Bw Barasa

Habari zinazohusiana na hii

Wachuuzi wa ahadi hewa

Raila amtetea Ruto