MATHEKA: Shule ziimarishe mawasiliano kati yao na wazazi, wanafunzi

Na BENSON MATHEKA

VISA vya kuchoma mabweni shuleni ambavyo vimeripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini vinahuzunisha mno.

Wanafunzi wamekuwa wakichoma mabweni katika shule zao na kuharibu mali ya mamilioni ya pesa hatua ambayo inaongezea wazazi wao mzigo wa kugharimia hasara wanayosababisha.

Hata hivyo, visa hivi vinaonyesha kuna pengo katika mawasiliano kati ya walimu na wanafunzi, wanafunzi na wazazi na wazazi na walimu. Katika baadhi ya shule, wanafunzi wamekuwa wakichukua sheria mikononi mwao wakidai walimu wamekuwa wakipuuza malalamishi yao. Ingawa sio chochote wanachotaka wanafaa kutimizwa, kuna haja ya walimu wakuu kusikiliza wanafunzi na kutafuta suluhu ya malalamishi yao badala ya kuwapuuza.

Walimu pia wanafaa kuimarisha mbinu za kuwasiliana na wazazi ili wasaidiane kushughulikia malalamishi ya wanafunzi na matatizo yakizuka shuleni.

Baadhi ya walimu wakuu huwa wanawapuuza wazazi wanapowasilisha malalamishi wanayopata kutoka kwa wanafunzi, na pia kuna wazazi wanaopuuza malalamishi ya walimu kuhusu tabia za watoto wao.

Ikizingatiwa kwamba wanafunzi huwa wanatoka matabaka mbali mbali, kuna haja ya kupalilia mazingira ya usawa shuleni bila kuonyesha upendeleo na ubaguzi.

Katika baadhi ya shule, wanafunzi kutoka familia masikini huwa wanalalamika kuwa walimu huwa wanawapendelea wenzao kutoka familia za matajiri na katika baadhi ya shule, kuna walimu wanaowachochea wanafunzi kutoka familia za mabwenyenye kudharau wale wanaotoka familia zisizojiweza.

Haya ni baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha taharuki na ghasia katika shule za sekondari ikizingatiwa umri wa wanafunzi. Katika shule ambazo kuna mifumo thabiti ya mawasiliano katika ya walimu, wanafunzi na wazazi, ghasia huwa ni nadra kuripotiwa. Mawasiliano haya huwa yanazaa ushirikiano ambao huwa unachangia upaliliaji wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi. Katika shule ambazo wanafunzi huwa wanadumisha nidhamu ya hali ya juu, matokeo huwa mazuri.

Wanafunzi wanafaa kukumbushwa kuwa, sababu yao kuwa shuleni ni kuwaandaa kwa maisha ya siku zijazo na sio kwa faida ya walimu na wazazi.

Hii inawezekana kukiwa na uhusiano mwema kati yao, walimu na wazazi wao jambo linalowezekana kupitia ushirikiano. Ghasia hizi zikiendelea, zitavuruga elimu nchini na matokeo yake yataathiri jamii. Inasitikisha kwamba ghasia hizi zinaendelea kukiwa na ripoti nyingi kuhusu chanzo cha ghasia katika shule ishara kwamba utekelezaji wake ni wa kutiliwa shaka.

Habari zinazohusiana na hii