KAMAU: Uhuru ajaribu kurejesha utulivu katika ngome yake

Na WANDERI KAMAU

KATIKA mila na desturi za Kiafrika, ni vizuri kwa watoto kuonyesha hekima kwa wazazi wao.

Ndio uhalisia uliopo hata kwenye mafundisho ya kidini. Wazazi huwa kama ‘mungu’ wa pili kwa watoto wao.

Ni kutokana na hadhi hiyo kubwa ya wazazi ambapo Mungu ameeleza adhabu kali kwa wale ambao wanawakosea heshima wazazi wao kwa namna yoyote ile.

Taswira hiyo huwepo karibu katika kila nyanja zote kwenye maisha tunayoishi hapa duniani; zikiwemo siasa.

Wanasiasa wachanga daima hushauriwa kuwatii wakubwa wao.

Vivyo hivyo, wanasiasa wenye uzoefu wanapaswa kuwa kielelezo chema kwa viongozi wanaochipuka.

Ndiyo hali itakavyoshuhudiwa leo, Rais Uhuru Kenyatta atakapokutana na viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri.

Kwa miaka mitatu sasa, ukanda huo umegeuka kuwa jukwaa la mafarakano. Wanasiasa wamekuwa wakigeukiana wao kwa wao kulingana na mirengo ya kisiasa wanayoegemea.

Sababu kuu ya migawanyiko hiyo ni harakati za urithi wa Rais Kenyatta, anayetarajiwa kung’atuka uongozini mwaka ujao. Ni migawanyiko ambayo imezua uhasama, chuki, ushindani usiofaa na hata maafa!

Kiafrika, eneo hilo limegeuka kama nyumba iliyokosa mwongozo.

Nyumba ambayo baba hana usemi, ama ameamua kunyamaza kimakusudi huku wanawe wakizozana na kuelekezeana cheche za matusi bila kujali uwepo wake.

Ni taswira ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya sitini wakati hayati Mzee Jomo Kenyatta alikuwa msemaji wake mkuu kisiasa. Vile vile, haikujitokeza wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki kati ya 2002 na 2013.

Anapokutana na viongozi hao leo, wito mkuu kwa Rais Kenyatta ni kutumia ushawishi wake kutuliza hali na kudhibiti ushindani wa siasa za urithi.

Si vizuri Rais Kenyatta kunyamaza wakati ngome yake imegeuka kama mnara wa Babeli. Ingawa ni haki ya wanasiasa kuendesha siasa zao, Rais anapaswa kutumia mkutano huo kurejesha uthabiti na utulivu uliokuwepo awali.

Huu ni wakati wake kushusha msimamo mkali na maonyo ambayo amekuwa akitoa akiwaelekezea baadhi ya wanasiasa, na badala yake kukubali maoni yao. Ni wakati wa kudhihirisha mfano mwema kama ‘baba’ kwa watoto wake.

Hili litahakikisha ametuliza mazingira ya kisiasa na kupata nafasi bora kukamilisha utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Ili kutimiza hayo, anapaswa kukoma kuupendelea mrengo wowote wa kisiasa, kama baba afanyavyo wakati anasuluhisha tofauti baina ya wanawe.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii