• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
WANTO WARUI: TSC imejifunga kibwebwe kuporomosha KNUT kabisa!

WANTO WARUI: TSC imejifunga kibwebwe kuporomosha KNUT kabisa!

Na WANTO WARUI

Tume ya kuajiri Walimu nchini (TSC) imetoa meno yake yote nje kuhakikisha kuwa inang’ata adui yake wa miaka mingi, KNUT (Chama cha Kutetea Maslahi ya walimu Nchini) bila huruma.

Mvutano ambao umekuwapo kati ya TSC na KNUT huenda ukafikia kikomo baada ya TSC kugundua na kuanzisha mbinu mpya za kukabiliana na walimu ambao ni wanachama wa KNUT.

Kwa muda mrefu sasa, KNUT na TSC zimekuwa maji na mafuta. Tangu kuundwa kwa chama hiki cha KNUT mwaka wa 1957, chini ya katibu wake wa kwanza Joseph Kioni, serikali haijawa na amani hasa pale ambapo KNUT ilifikiria kuwa walimu hawatimiziwi mahitaji yao. Mwaka baada ya mwaka KNUT imekuwa ikitishia serikali kwa migomo.

Itakumbukwa kuwa KNUT ilifanya mgomo wake wa kwanza 1963, kabla Kenya haijapata uhuru wake. Tangu wakati huo, chama hiki cha walimu kimekuwa kikichezeana mchezo wa paka na panya na serikali kuhusu mishahara ya walimu.

Vitisho vya migomo na wakati mwingine kufaulu kwa migomo hiyo limekuwa jambo ambalo limeathiri pakubwa sekta ya elimu nchini.

Kuwepo kwa mivuto hii baina ya TSC na KNUT ambayo imesababisha migomo kadhaa ya walimu nchini huenda ni mojawapo ya sababu ambazo zinawaelekeza wanafunzi kufuata mtindo huo wa kugoma na kusababisha hasara kubwa katika shule zetu.

Mnamo mwaka wa 1997, walimu waliweka ‘majembe’ yao chini kwa muda wa siku 12. Mnamo September 18, 2015, serikali ililazimika kusimamisha masomo baada ya walimu kugoma tangu Agosti 31, mwaka huo shule zilipofunguliwa. Ingawa serikali imekuwa ikijaribu kwa udi na ambari kutatua matatizo haya ya migomo ya walimu, suluhisho la kudumu halijapatikana.

Lakini sasa serikali kupitia TSC inaonekana kama imeamua kutolea KNUT makali yake na kuifunza funzo ambalo halitasahaulika. Mvutano wa KNUT na TSC wa hivi majuzi ambao umeishia mahakamani mara kadhaa huenda ukaishia kusambaratisha KNUT kabisa.

Mgogoro huu kuhusu nyongeza za mishahara ya walimu, kupandishwa vyeo na kuhamishwa kazini umekuwa mwiba mchungu sasa kwa KNUT.Idadi ya walimu ambao ni wanachama wa KNUT sasa ni 23,000 tu kutoka kwa idadi kubwa ya hapo awali ya zaidi ya walimu 130,000.

Tume hiyo ya kuajiri walimu iliwawekea masharti walimu ambao ni wanachama wa KNUT ya kutowaongezea mishahara au kuwapandisha vyeo endapo wataendelea kuwa katika KNUT, jambo ambalo limeonekana likihamishia walimu kwa chama cha KUPPET na wengine kukaa bila chama cha kuwawakilisha.

Hatua hii ya TSC inaonekana kama ndilo pigo kubwa zaidi kwa KNUT huku katibu wake mkuu, mbunge Bw Wilson Sossion akiachwa kujitazamia tu chama cha KNUT kikiporomoka.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Rais aingilie kati, azime joto kali la...

Walimu waililia serikali iwalinde dhidi ya ugaidi