• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Pingamizi kwa Kidero akitaka kuwika kijijini

Pingamizi kwa Kidero akitaka kuwika kijijini

Na GEORGE ODIWUOR

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero anakabiliwa na wakati mgumu kushawishi wapigakura sababu zake za kutaka kuwania ugavana Homa Bay baada ya kushindwa Nairobi katika uchaguzi uliopita.

Wanasiasa wa Kaunti ya Homa Bay wameanza kumpiga vita na kusema hafai kuwa gavana wa kaunti hiyo ya ‘mashambani’.

Dkt Kidero ametangaza azma ya kugombea kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao lakini anapata pingamizi kali kutoka kwa wanasiasa wanaotaka kumrithi Gavana Cyprian Awiti.

Mwanasiasa wa hivi punde kumshambulia Dkt Kidero ni aliyekuwa mbunge wa Kasipul Oyugi Magwanga ambaye alitofautiana naye kuhusu uamuzi wake wa kutaka kugombea kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Magwanga ametangaza azma ya kugombea kiti hicho alichopoteza kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 baada ya kushindwa na Awiti.

Bw Magwanga alisema kwamba Dkt Kidero anajishusha hadhi kwa kugombea ugavana kaunti ya Homa Bay.

Kulingana na Bw Magwanga, mipango ya Dkt Kidero ya kugombea kiti hicho itashusha sifa zake iwapo atashindwa.

“Wewe ni mwanasiasa wa heshima ambaye ulituwakilisha vyema kama jamii ulipokuwa gavana wa Nairobi. Utashusha hadhi yako kwa kugombea ugavana wa Kaunti ya Homa Bay,” Bw Magwanga alimweleza Dkt Kidero walipokutana katika mazishi kaunti ya Homa Bay.

Alimlinganisha Dkt Kidero na mwana mkomavu wa jamii ya Waluo ambaye amejenga boma lake baada ya kuhama kwa wazazi wake.

“Ni kinyume cha desturi za jamii ya Waluo kwa mwana kama huyo kuacha boma lake na kurudi kuishi na wazazi wake tena,” alisema mbunge huyo wa zamani.

Akimjibu, Dkt Kidero alijaribu kuwashawishi wakazi wa Homa Bay kwamba yeye ni mwana wao na anafaa kupatiwa nafasi ya kugombea kiti cha ugavana.

Alipuuza kauli ya Magwanga akisema kwamba alienda Nairobi kutafuta kazi kama mwanamume yeyote yule kutoka Homa Bay anavyoweza kufanya kazi katika kaunti nyingine.

“Baadhi ya watu wanasema kwamba sitoki kaunti ya Homa Bay. Watu wote wa familia yangu akiwemo mke wangu wanatoka Homa Bay na kwa hivyo mimi natoka hapa. Nilizaliwa katika kaunti ya Homa Bay na nikaenda Nairobi kutafuta kazi. Sasa nimerudi na ninataka kuwa gavana wenu,” aliwaambia wakazi.

Dkt Kidero alisema kwamba anabaguliwa kwa kutopatiwa nafasi ya kugombea kiti cha kisiasa anachotaka.

“Sitakubali presha za kutaka nirudi Nairobi. Nimefanya uamuzi wa kugombea Homa Bay,” alisema.

Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang na mbunge wa Rangwe Lillian Gogo pia walihudhuria mazishi hayo.

You can share this post!

Kiplagat, kigogo wa enzi ya Moi aliyedaiwa kope

Karua: BBI ni hujuma kwa Katiba