• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Barabara ya Thika-Gatuanyaga kukamilika katika kipindi cha miezi 30

Barabara ya Thika-Gatuanyaga kukamilika katika kipindi cha miezi 30

Na LAWRENCE ONGARO

BARABARA kutoka Thika mjini hadi eneo la Gatuanyaga katika Kaunti ya Kiambu itanufaisha wafanyabiashara wengi mara itakapokamilika.

Kulingana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Barabara za Mijini (KURA), Bw Benjamin Asin, barabara hiyo ya umbali wa kilomita 17 itagharimu takribani Sh1.7 bilioni na kukamilika baada ya miezi 30 ijayo.

Alisema changamoto wanazopitia katika mradi huo ni kupasuka kwa mabomba ya maji ardhini wakati wa ukarabati huo, na jinsi ya kufuatiliza nyaya za umeme katika maeneo ya mradi huo.

“Tunaelewa vyema kuna changa moto nyingi lakini tutafanya juhudi kukabiliana nazo,” alisema Bw Asin.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana alipozuru mji wa Thika kujionea mwenyewe jinsi ukarabati huo unavyoendelea.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina ambaye aliandamana na mkurugenzi huyo aliwashauri wakazi wa eneo la Kang’oki walionunua ardhi mahali hapo wahame haraka kwa sababu wahandisi hao watabomo nyumba zao bila kujali.

Wakazi hao walipewa muda wa miezi miwili kufuata magizo hayo.

“Wakazi walionunua vipande vya ardhi pahala hapo washirikiane na KURA ili waondoke kwa amani,” alisema Bw Wainaina.

Alitaja mradi huo kuwa wa kupongezwa kwa sababu wafanyabiashara wengi watanufaika pakubwa kutokana na barabara nzuri ya kisasa.

Alitoa wito kwa wakazi wa Gatuanyaga wasiuze vipande vyao vya ardhi kwa wageni kwa sababu baada ya kukamilika kwa barbara hiyo bei ya ardhi itapanda.

Mhudumu wa bodaboda eneo hilo, Bw Joseph Ndung’ u, alisema kwa muda mrefu wamefanya biashara ya hasara sababu ikiwa ni ubovu wa barabara.

“Nilikuwa nanunua miguu ya pikipiki kila mwezi kwa sababu ya magurudumu kupasuka kila mara,” alisema Bw Ndung’u.

Naye Mzee wa Kijiji cha Gatuanyaga Bw John Mwangi alipendekeza kuwa vijana wa kijiji hicho wapewe kibarua badala ya kutoa wafanyakazi maeneo mengine.

“Tunaiomba KURA ifanye hima kuona ya kwamba watu wa kwanza kuajiriwa wawe watoto wetu wa hapa,” alisema Bw Mwangi.

  • Tags

You can share this post!

Inter Milan wapiga AC Milan na kufungua mwanya wa pointi...

BI TAIFA FEBRUARI 22, 2021