• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Mwalimu amkata mwenzake wakipigania msichana wa chuo

Mwalimu amkata mwenzake wakipigania msichana wa chuo

Na GEORGE MUNENE

POLISI katika Kaunti ya Kirinyaga wanamzuilia mwalimu aliyemjeruhi mwenzake kwa kutumia upanga mnamo Jumanne, kwenye kisa kinachodaiwa kuwa mzozo wa kimapenzi.

Mwathiriwa, aliyetambuliwa kama Alfonse Orina, 26, alipata majeraha mabaya kichwani na mikononi mwake. Kisa hicho kilifanyika katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Karoti, Kirinyaga.

Kwanza Mwathiriwa alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti-ndogo ya Kimbimbi, alikolazwa akiwa katika hali mahututi.

Baadaye, alipelekwa katika hospitali ya kibinafsi ya Afya Bora kupokea matibabu maalum, baada ya hali yake kudorora.

Kisa hicho kilisimamisha shughuli za masomo katika shule hiyo kwa muda, ambapo wanafunzi walitoka madarasani kumtazama mwalimu wao aliyejeruhiwa akipelekwa hospitalini.

Walioshuhudia walisema kuwa Bw Orina alikuwa kwenye chumba cha walimu, wakati mwalimu mwenzake alipoingia kwa hasira akiwa amebeba upanga, akidai mwathiriwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenziwe.

Msichana anayezozaniwa ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo kikuu na kwa sasa anafanya mafunzo ya nyanjani (uanagenzi) shuleni humo.

Mshambuliaji alimgonga mwathiriwa kichwani mara mbili, ndipo Bw Orina akalazimika kumkabili pia. Hata hivyo, mwathiriwa alijeruhiwa vibaya mikononi mwake, alipojaribu kumzuia mwenzake kumshambulia.

Walimu waliofika walimnusuru Bw Orina na kumkimbiza hospitalini akiwa ashapoteza fahamu.

Walipofika hospitalini, mwathiriwa alipelekwa moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji kwani vidole vyake vilikuwa vimekatika kwa majeraha makubwa. Madaktari katika hospitali hiyo walisema atapigwa picha kichwani mwake kubaini ikiwa ubongo wake uliathirika kwa namna yoyote ile.

“Ana majeraha mabaya kichwani mwake, hivyo itabidi apigwe picha kubaini yalikofikia,” wakasema madaktari. Kufuatia kisa hicho, polisi walimkamata mshukiwa na kumzuilia katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru ili kuhojiwa. Polisi waliozuru eneo la mkasa walitaja tukio hilo kama la “kusikitisha”.

“Damu ilikuwa imetapakaa kwenye vitabu, kwenye nyua, sakafuni kati na maeneo mengine katika chumba cha walimu. Hiyo ni ishara kuwa mwathiriwa alijeruhiwa vibaya sana,” akasema mmoja wa polisi wanaochunguza tukio hilo.

Mkuu wa Polisi katika Kaunti-ndogo ya Mwea Mashariki, Bw Daniel Kavita, alisema mshukiwa atafunguliwa mashtaka ya jaribio la kuua baada ya uchunguzi kukamilika.

Alisema watatumia upanga huo kama ushahidi.

You can share this post!

Echesa anaswa akimzaba kofi afisa wa IEBC katika uchaguzi...

Kingi amzima Raila