• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
BENSON MATHEKA: Kiini cha Raila kuhofia vyama vya Pwani na Magharibi kuungana

BENSON MATHEKA: Kiini cha Raila kuhofia vyama vya Pwani na Magharibi kuungana

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga anahofia kwamba kuibuka kwa miungano ya vyama vya kisiasa eneo la Pwani na Magharibi ya nchi kutapunguza umaarufu ambao amekuwa akifurahia maeneo hayo tangu 2007 anapojiandaa kugombea urais kwa mara ya tano.

Bw Odinga amekuwa akikosoa viongozi wa Pwani na Magharibi mwa nchi wanapopanga kuunda vyama vyenye nguvu au kuunganisha vyama vyao akisema Kenya inahitaji vyama vya kitaifa na si vya kimaeneo au kikabila.

Wiki hii, alitofautiana paruwanja na Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi ambaye amekuwa akiongoza juhudi za kutaka eneo la Pwani kuwa na chama cha kisiasa kitakachowakilisha maslahi yao akisema ni tishio kwa umoja wa taifa.

Bw Odinga pia amekuwa akipinga juhudi za Bw Musalia Mudavadi na seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuunganisha vyama vyao vya Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya akisema wanalenga siasa za kikabila.

ANC na Ford Kenya vina wafuasi wengi eneo la Magharibi ambalo sawa na Pwani limekuwa likimpigia Bw Odinga kura kwa wingi tangu 2007.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kwamba waziri huyo mkuu wa zamani anahofia kuwa umaarufu wake utapungua pakubwa maeneo hayo uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

“Bw Odinga anahisi kwamba kuungana kwa wakazi nyuma ya kigogo wa siasa kutoka maeneo hayo kutamnyima umaarufu ambao amefurahia kwa zaidi ya miaka 13 sasa hasa ikitiliwa maanani Naibu Rais William Ruto ambaye kwa sasa ndiye mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 amepenyeza katika ngome zake,” asema mdadisi wa siasa Joseph Kiilu.

Anasema Bw Odinga anajua kwamba maeneo ya Pwani na Magharibi yakimponyoka, itakuwa mlima kwake kushinda urais.

“Nguvu za Raila nje ya Nyanza ni Magharibi ya Kenya, Pwani na Nairobi. Amekuwa akitumia migawanyiko ya vigogo wa kisiasa eneo la Magharibi kutawala kura za jamii ya Mulembe na hii ndiyo sababu amekuwa akipinga muungano wa vyama vya ANC na Ford Kenya,” asema.

Eneo la Pwani halijakuwa na chama kimoja chenye nguvu licha ya kuwa na vyama vinne vilivyoanzia ukanda huo. Vyama hivyo ni Kadu Asili, Shirikisho, Republican Congress na Umoja Summit.

Wadadisi wanasema kwamba umaarufu wa Bw Odinga katika maeneo ya Pwani na Magharibi umetokana na ushirika wake na vigogo wa kisiasa maeneo hayo na kuungana kwao kunaweza kuwa pigo kwake hasa ikizingatiwa kwamba uchaguzi mkuu ujao unatarajiwa kuwa wenye ushindani mkubwa.

“Hii ndiyo sababu anadai viongozi wa maeneo hayo wanapanga kuunda vyama vya kimaeneo au kikabila na kusahau kwamba kabla ya chama kusajiliwa, lazima kiwe na sura ya kitaifa. Hata hivyo, hakuna chama kisicho na ngome yake kwa kutegemea sera na anakotoka kiongozi wake,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Kasuku.

Kwa mujibu wa Bw Kingi, hakuna mipango ya kubuni chama kipya cha eneo la Pwani anavyodai Bw Odinga bali wanacholenga ni kuleta pamoja vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi Pwani kushinikiza ajenda za kisiasa na kiuchumi za eneo hilo.

“Kama viongozi wa Pwani, hatutaki kutenga eneo letu. Watu wanafaa kuruhusiwa kubuni miungano na kwa kufanya hivi tutaheshimiana,” asema Kingi

Bw Kasuku asema hakuna kosa lolote kwa eneo kuungana na kwa kupinga hatua hiyo, Bw Odinga anafanya wakazi wa Pwani wanaohisi wamepuuzwa kujitenga naye.

“Kauli ya Bw Raila inadhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa viongozi wanaohujumu umoja wa watu wa Pwani ambao wamekuwa wakiteseka kwa kukosa kuzungumza kwa sauti moja,” asema.

Kauli hii ni sawa na ya Bw Mudavadi ambaye amenukuliwa akisema kwamba kuna watu wanaonufaika na kugawanyika wa jamii ya Mulembe.

Bw Kasuku anasema kwamba kinachomkosesha Bw Odinga usingizi ni kuzinduka kwa vigogo wa kisiasa eneo la Pwani na Magharibi.

“Anahisi kwamba kuna nguvu katika umoja na siasa za urithi za mwaka wa 2022 zinapokaribia, kuna hatari ya wanasiasa aliotegemea kutoka maeneo hayo kumtema na kujiunga na mpinzani wake,” asema.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba maeneo haya mawili- Pwani na Magharibi- ndio uhai wa kisiasa wa Bw Odinga nje ya Nyanza na yakimpa kisogo kisiasa, azma yake ya kuingia ikulu itabaki ndoto.

“Ukweli usiopingika ni kuwa bila kuungwa mkono na wapigakura wa maeneo ya Pwani na Magharibi, nafasi ya Bw Odinga kushinda urais itapungua pakubwa. Hii ndiyo sababu anapigana kufa kupona kuhakikisha maeneo haya hayamponyoki kwenye uchaguzi mkuu ujao,” asema Bw Kiilu.

Anasema kuungana kwa Bw Mudavadi na Bw Wetangula kunaweza kubadilisha mkondo na kuzua wimbi jipya la kisiasa eneo la Magharibi na kumfanya Bw Odinga kutegemea Pwani nje ya Nyanza.

Bw Kingi anasema kwamba wakati umefika Wapwani kuungana kutetea maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi na wanapochukua hatua hiyo hawafai kutishwa.

“Vyama vya kisiasa maeneo mengine vinaungana. Mbona inakuwa tisho tukisema Pwani tuungane?” anahoji na kutoa mfano wa Bw Musalia na Bw Wetangula.

You can share this post!

JAMVI: Hofu jahazi la Ruto limeanza kupasua nyufa Mlima...

Chanjo ya corona isiwe cheti kuamsha ufuska