• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
JAMVI: Hofu jahazi la Ruto limeanza kupasua nyufa Mlima Kenya

JAMVI: Hofu jahazi la Ruto limeanza kupasua nyufa Mlima Kenya

Na WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka kuhusu mustakabali wa “urafiki” kati ya Naibu Rais William Ruto na washirika wake katika ukanda wa Mlima Kenya, baada ya baadhi yao kubuni vyama mbadala vya kisiasa tuelekeapo 2022.

Tashwishi hizo pia zinaibuka ikizingatiwa kuwa tayari, Dkt Ruto amehusishwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) anachotarajiwa kukitumia kuwania urais.

Miongoni mwa wandani ambao wamebuni vyama hivyo ni aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, anayeongoza chama cha The Service Party (TSP), mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria (People’s Empowerment Party-PEP) na Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kirinyaga, Wangui Ngirichi, anayehusishwa na chama cha Citizen Convention Party (CCP). Chama hicho kinadaiwa kuongozwa na mumewe Bi Ngirichi, Andrew Ngirichi.

Aidha, Bw Kuria amekuwa akiwasimamisha wagombeaji wa udiwani katika chaguzi kadhaa nchini. Kwa mfano, chama cha PEP chake Bw Kuria kilikuwa na wagombea katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika wadi za Huruma (Kaunti ya Uasin Gishu) na London (Kaunti ya Nakuru) mnamo Alhamisi.

Wagombea hao ni Bernard Maina (wadi ya London) na Francis Maina (wadi ya Huruma).

Bw Kuria hata alifika katika katika maeneo hayo na kuwafanyia kampeni, na kukosa kujiunga na misafara iliyokuwa ikiwapigia debe wawaniaji walioungwa mkono na Dkt Ruto.

Madai yameibuka kwamba huenda mbunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu) pia anapanga kubuni chama chake cha kisiasa.

Mbali na vyama hivyo, baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kama Seneta Kindiki Kithure (Tharaka Nithi) wamesema kuwa hatawajiunga na UDA “vivi hivi tu” bali watatafuta njia zao huru za kisiasa ili “kuepuka yale waliyopitia katika Jubilee” ambapo zaidi ya vyama kumi vya kisiasa vilivunjwa ili kubuni chama hicho.

“Hatuwezi kumsaliti Dkt Ruto hata kidogo. Lazima tuhakikishe amepata uungwaji mkono Mlimani, kama tulivyomwahidi wakati wa kubuniwa kwa Muungano wa Jubilee mnamo 2012,” akasema Prof Kindiki.

Licha ya kusisitiza hatua hiyo hailengi “kumgeuka” Dkt Ruto, wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa mwelekeo huo unapaswa kumfungua macho Dkt Ruto kuhusu mwelekeo wa uungwaji mkono wake katika ukanda huo.

Tayari, UDA imetangaza kubuni mkataba wa kisiasa na TSP, hali ambayo inaelezwa kuongeza mvutano wa kichinichini katika kundi la ‘Tangatanga’, ambalo limekuwa nguzo na sauti kuu ya Dkt Ruto katika eneo hilo.

Wadadisi wanasema mwelekeo huo unaonyesha kuwa huenda Bw Kiunjuri “akawa na usemi mkubwa katika kambi ya Dkt Ruto” ikilinganishwa na wabunge ambao wamekuwa wakimsaidia kuendesha kampeni zake katika sehemu mbalimbali nchini.

“Mvutano ambao huenda ukaibuka na ukayumbisha merikebu ya kisiasa ya Dkt Ruto Mlimani ni hisia za kuwatenga washirika wake wa karibu kama wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara) kati ya wengine licha ya kumsaidia kuendesha kampeni zake,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za ukanda huo.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Uchina isipime corona kwa njia ya...

BENSON MATHEKA: Kiini cha Raila kuhofia vyama vya Pwani na...