• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wabunge wandani wa Ruto wapokonywa walinzi, bunduki

Wabunge wandani wa Ruto wapokonywa walinzi, bunduki

VINCENT ACHUKA na CHARLES WASONGA

USALAMA wa wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto sasa uko hatarini baada ya kupokonywa walinzi na leseni zao za bunduki kwa kutuhumiwa kuchochea fujo wakati wa chaguzi ndogo zilifanyika Alhamisi.

Kwenye taarifa Bodi ya Kutoa Leseni za Bunduki (FLB) ilisema kuwa imefutulia leseni za bunduki za wabunge; Didmus Barasa (Kimilili) na Fred Kapondi (Mlima Elgon).

Taarifa hiyo iliyotolewa Machi 5 na kutiwa saini na mwenyekiti wa bodi hiyo Charles Mukindia, ilisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia amri ya Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai na baada ya uchanganuzi wa mienendo ya utovu wa nidhamu ya wanasiasa iliyoshuhudiwa katika chaguzi katika maeneo bunge ya Kabuchai na Matungu.

Wabunge hao waliamriwa warejeshe leseni za bunduki na bunduki “zikiwemo risasi” walizonazo kwa bodi hiyo au kituo cha polisi kilichoko karibu ndani ya saa 24.

“Ukikaidi amri hii utachukuliwa hatua kali na bodi hii au asasi zingine za kisheria,” Bw Mukindia akaonya.

Aliongeza za kuwa bodi hiyo itaendelea kufuatilia visa vya matumizi mabaya ya silaha hizo na watu ambao wamepewa lesi za kuzimiliki.

Mnamo Jumapili Bw Barasa aliambia Taifa Leo kuwa ameagizwa na kurejesha leseni na bunduki yaka katika kituo cha polisi kilichoko karibu au katika afisi za LFB.

“Kando na hayo mlinzi wangu hakuripoti kazini Jumamosi asubuhi. Aliniambia amepokea agizo kutoka kwa wakubwa wake katika Tume ya Kitaifa ya Polisi (NPSC) arejeshe aripoti katika makao makuu ili apewe majukumu mengine,” akasema.

Wanasiasa wengine waliopokonywa bunduki zao ni Seneta wa Nandi Samson Cherargei na wabunge Nelson Koech (Belgut), Fred Kapondi (Mlima Elgon) na Wilson Kogo (Chesumei).

Mbw Barasa, Cherargei, Koech na Kogo Ijumaa walifikishwa katika mahakama ya Bungoma na kushtakiwa kwa kosa la kupanga kuzua ghasia katika uchaguzi mdogo wa Kabuchai. Ilidaiwa kuwa silaha butu silipatikana katika magari ya wanasiasa hao waliofika huku kuhudumu kama maajenti wa mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Evans Kakai.

Walikana makosa hayo na kuachiliwa huru kwa dhamani ya Sh50,000 pesa taslim na mdhamini ya Sh100,000. Kesi yao itasikizwa mnamo Aprili 4, 2021.

Seneta Maalum Millicent Omanga pia alilalamika Ijumaa kwamba alipokonywa mlinzi lakini akadai kuwa hatishwi na hatua hiyo kwa sababu “Mlinzi wangu Mkuu ni Mungu.”

Hatua hiyo ilichukuliwa dhidi ya wanasiasa hao baada ya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuonya kwamba hatua kali itachukuliwa dhidi ya wanasiasa wanaochochea fujo katika shughuli za kisiasa. Vile vile, aliamuru kwamba wanasiasa kama hao wapokonywe bunduki zao “wasije wakasababisha madhara makubwa zaidi.”

Vile vile, Dkt Matiang’i alisema serikali itasaka idhini ya Mahakama ili wanasiasa kama hao wazuiwe kushikilia nafasi za umma kwa msingi ya kukiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili na uongozi bora.

Tishio sawa na hili lilitolewa na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Jumamosi.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tutajinasua vipi kutoka kwa usahaulifu wetu?

Kituyi arejea nyumbani kusaka baraka za urais