• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Moi ndiye mrithi wa Uhuru, Kanu yasema

Moi ndiye mrithi wa Uhuru, Kanu yasema

Na OSCAR KAKAI

CHAMA cha Kanu kimeshikilia kuwa mwenyekiti wake Gideon Moi ndiye atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2022.

Chama hicho pia kimetoa orodha ya viongozi ambao wataunga mkono Bw Moi katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket wikendi alisema kuwa ataungana na viongozi wa vyama Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Gavana wa Mombasa Hasan Joho.

Gavana huyo wa Mombasa tayari ametangaza kuwa atawania urais kupitia chama cha ODM.

Bw Joho, wiki iliyopita, alitangaza kuwa atamuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga endapo atambwaga katika kura za mchujo za chama hicho.

“Bw Gideon tayari amewaweka kibindoni vinara wa eneo la Magharibi, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula. Katika eneo la Mashariki anashirikiana na Bw Musyoka na ukanda wa Pwani atashirikiana na Gavana Joho kati ya wengineo,” akasema Bw Kamket.

Mbunge huyo alikuwa akizungumza Jumamosi katika hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya makundi ya wanawake iliyoongozwa na Bw Moi katika Shule ya Msingi ya Psiwo, Ortum, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Bw Moi alipokuwa akizungumza Jumapili katika hafla ya kumtawaza Askofu wa Kanisa la AIPCA, Kaunti ya Kiambu, alikwepa kuzungumzia siasa za 2022 na kuahidi kutangaza ikiwa atawania urais au la baada ya kupitishwa kwa Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Lakini Jumamosi, Bw Moi alimtaka Dkt Ruto kurejea nyumbani Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu, aende “akauze kuku”.

Bw Moi alisema kuwa hatua ya mabunge ya Kaunti zinazozidi 40 kuunga mkono mswada wa BBI, ilikuwa ishara kwamba Dkt Ruto hana ushawishi wa kisiasa nchini.

“Naibu wa Rais amekuwa akijipiga kifua na kujigamba kuwa angesambaratisha BBI lakini sasa anafaa kukubali uamuzi wa Wakenya na kufunganya virago vyake aende Sugoi kufuga kuku,” akasema Seneta wa Baringo.

Naibu wa Rais, Dkt Ruto ambaye ametangaza kuwania urais 2022, na Seneta wa Baringo wamekuwa wakishindania ubabe wa kisiasa wa eneo la Bonde la Ufa.

“Tusichanganye BBI na siasa za 2022. Kuna baadhi ya wanasiasa wameanza kampeni za mwaka ujao na kusahau masaibu ya wananchi,” akasema Bw Moi.

Bw Moi alibarikiwa na wazee wa jamii ya Wapokot huku wakimtakia heri njema katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

You can share this post!

Gor Mahia yanyamazishwa 2-0 na wageni KCB

Fulham wawika ugenini na kuendeleza masaibu ya Liverpool...