• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Gor Mahia yanyamazishwa 2-0 na wageni KCB

Gor Mahia yanyamazishwa 2-0 na wageni KCB

Na GEOFFREY ANENE

WIKI moja baada kutembelea kaburi la mganga maarufu Gor Mahia katika kaunti ya Homabay, kutafuta baraka zake, klabu ya Gor Mahia ilinyamazishwa 2-0 na wageni wao KCB kwenye Ligi Kuu, Jumapili.

Katika mchuano huo wa 11 wa Gor na 14 kwa KCB uwanjani Moi Kasarani, mabingwa watetezi Gor walizamishwa na mabao ya Dennis Simiyu na Victor Omondi yaliyopatikana katika dakika 15 za mwisho.

Timu hizo zilijibwaga uwanjani zikitafuta ushindi wa kwanza baada ya kuokota alama moja katika mechi tatu zilizopita.

Makipa Bonface Oluoch (Gor) na Gabriel Andika (KCB) walihakikisha timu zao zinaenda mapumzikoni bila kufungwa baada ya kufanya kazi kubwa michumani.

Dakika sita baada ya mshambuliaji wa Gor, Tito Okelo kupoteza nafasi nzuri, wanabenki wa KCB walifungua ukurasa wa mabao kupitia Simiyu dakika ya 75.

Mambo hayakuwa tofauti kabla ya Omondi kuongeza bao la pili kupitia penalti dakika ya 85. Oluoch aliangusha Omondi ndani ya kisanduku na kutunuku KCB nafasi hiyo nzuri ya kuzamisha kabisa chombo cha mabingwa hao wa mataji 19, ambao kampeni yao ya kutwaa kombe hilo kwa msimu wa tano mfululizo inaonekana kufifia mapema.

Kabla ya penalti hiyo, mshambuliaji wa Gor, Clifton Miheso alikuwa amesukuma shuti kali dakika ya 82 lililopanguliwa na Andika.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka 2011 KCB imefaulu kuchapa Gor ugenini baada ya kupoteza mechi tano na kutoka sare mara mbili katika saba zilizotangulia. Mara ya mwisho Gor ilikuwa imepoteza nyumbani dhidi ya KCB ilikuwa 1-0 Mei 16, 2010.

Gor Mahia alizaliwa mwaka 1796 na alikuwa na nguvu za kimiujiza ambazo zilimwezesha kuwalemea wapinzani. Alifariki mwaka 1922 akiwa na umri wa miaka 126. Kutembelea kaburi lake kunaaminika hulete baraka. Kwa mujibu wa tovuti ya Kenya & Beyond Safaris, kung’oa jani ama kuhamisha jiwe kutoka alikozikwa shujaa huyo bila ruhusa kunaaminika husababishia anayefanya hivyo balaa.

Timu hiyo ilipiga kambi mjini Homabay kabla ya mechi yake dhidi ya Kakamega Homeboyz. Gor ilishinda Homeboyz 2-1 mnamo Machi 3.

Kikosi cha Gor Mahia akiwemo kocha Mreno Carlos Manuel Vaz Pinto kilizuru kaburi la Gor Mahia baada ya timu hiyo kuwa na msururu wa matokeo duni ambapo ilibanduliwa kwenye Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Gor ilipoteza mechi dhidi ya Nzoia Sugar na Vihiga United ligini ambazo miaka iliyoenda ilitarajiwa kushinda kwa urahisi.

Gor inashikilia nafasi ya 13 kwa alama 16 kwenye ligi hiyo ya klabu 18 inayoongozwa na Tusker (alama 35) ikifuatiwa na KCB (29), AFC Leopards (28), Bandari (26) na Kariobangi Sharks (25) katika nafasi tano za kwanza. Itazuru Bidco United katika mechi ijayo mnamo Machi 10.

Nayo Homeboyz ilirukia nafasi ya 10 kutoka 13 baada ya kuchabanga mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United 2-1 katika mechi nyingine iliyochezewa katika uwanja wa nje wa Kasarani.

You can share this post!

Fumbo la kifo cha mwanamke baada ya kutembelewa na mseminari

Moi ndiye mrithi wa Uhuru, Kanu yasema