Zawadi ya basi kutoka kwa Ruto yazua utata Mlima Kenya

Na CHARLES WANYORO

MASWALI yameibuka kuhusu basi ambalo Naibu Rais William Ruto alitoa kwa shule moja ya upili katika eneo bunge la Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru, kama zawadi.Hii ni baada ya basi hilo kutwaliwa tena na kampuni iliyokuwa imeliuza.

Baadhi ya wakazi sasa wanadai kuwa uzinduzi wa basi hilo, siku 10 zilizopita, ulikuwa ni wa kuwahadaa kisiasa.Kulingana nao, basi hilo ambalo lilikabidhiwa Shule ya Upili ya Wasichana ya Kianjai lilitwaliwa na kukabidhiwa shule nyingine.

Lakini Mbunge wa eneo hilo, Bw John Mutunga, anasisitiza kuwa basi hilo lilikuwa limetolewa kiwandani kabla likamilike kutengenezwa, ilhali muda ulikuwa wayoyoma kwa Dkt Ruto kulipokeza kwa shule.

Naibu Rais alisimamia hafla ya kupokeza basi hilo wakati wa ziara yake ya siku tatu katika Kaunti ya Meru.Akiongea na wakazi katika eneo la Rwongo Rwa Nyaki alipokuwa amehudhuria hafla ya kutoa mahari kwa familia moja eneo hilo, Dkt Mutunga alisema basi hilo halikuwa limekamilika kuundwa kutokana na mlipuko wa corona.

Baadaye ilikubalika kwamba basi hilo liwasilishwe kwa shule hiyo jinsi lilivyokuwa ili Naibu Rais alikabidhi shule husika rasmi “kwa sababu ziara ya Dkt Ruto ilikuwa imepangwa miezi sita iliyopita” kisha lirudishwe kukamilishwa.

Dkt Mutunga alisema Naibu Rais alikuwa ametoa Sh3.5 milioni kwa ununuzi wa basi hilo, kama njia ya kutimiza ahadi aliyotoa kwa wanafunzi walipomtumbuiza katika uwanja wa michezo wa Urru, 2019.

“Kampuni (ambayo tumeibana jina kwa sababu za kisheria) ilitushauri kuendelea na hafla ya kulikabidhi basi hilo kwa shule hiyo, kisha uundaji wake ukamilishwe baadaye. Siwezi kumleta Dkt Ruto kutoka Nairobi kwa hafla bandia ilhali tumekuwa tukiiandaa kwa miezi sita iliyopita,” akasema.

Kurejeshwa kwa basi hilo Nairobi kulifichuliwa na kundi moja linalofahamika kama ‘Tigania Eye’, ambalo lilisema hatua hiyo ilichangiwa na hali kwamba afisi ya hazina ya CDF katika eneo hilo haikuwa imekamilisha malipo ya basi hilo.Wanachama wa kundi hilo walidai kuwa basi ambalo liliwasilishwa kwa Shule ya Upili ya Kianjai lilikuwa la shule nyingine.

Kulingana nao, hatua hiyo ilichukuliwa ili kuipa afisi ya Hazina ya CDF eneo bunge la Tigania Magharibi muda wa kulipa pesa zilizosalia za ununuzi wa basi jipya.

“Basi la shule ambalo lilipokezwa Shule ya Upili ya Wasichana ya Kianjai lilikuwa hadaa tupu, hafla hiyo iliandaliwa kwa manufaa ya kisiasa ya Dkt Mutunga na Naibu Rais. Tunatoa makataa ya hadi Jumamosi Machi 13, kwa wao kuhakikisha kuwa Shule ya Upili ya Wasichana ya Kianjai inapata basi ambalo iliahidiwa,” akasema Bw Ben Kiriinya aliyesoma taarifa ya kundi hilo awali.

Hata hivyo, Dkt Mutunga alisitiza kuwa madai ya kundi hilo yamechochewa kisiasa na kwamba basi hilo litawasilishwa kwa shule hiyo Jumatano wiki hii.

Habari zinazohusiana na hii

KONDOO WA RUTO MATAANI

Ruto amhepa Uhuru