• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
GWIJI WA WIKI: DKT EVANS MAKHULO

GWIJI WA WIKI: DKT EVANS MAKHULO

Na CHRIS ADUNGO

WATETEZI wa Kiswahili watafanya lugha hii ipendeze na ya kupendeka zaidi iwapo wataacha kulumbana, kujipiga vifua na kujipa lakabu za kutisha!

Ipo haja kwa wapenzi wa Kiswahili kushirikiana kwa lengo moja la kufaulisha makuzi, maendeleo na ustawi wa lugha hii katika sekta mbalimbali za jamii.

Wataalamu wa Kiswahili watawaliwe na kiu ya kusambaza maarifa, waendeleze msingi imara wa lugha na watoe mchango wa kuhimiza na kuchochea kasi ya kutekelezwa kwa malengo mahsusi katika nyanja za uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Nyaraka na stakabadhi muhimu za serikali zitafsiriwe kwa Kiswahili, hotuba zote za rais zitolewe kwa Kiswahili na vikao vya mabunge vidhihirishe kwamba Kiswahili kwa kweli ni lugha rasmi ya Kenya. Vinginevyo, urasmi wa Kiswahili utasalia tu kuwa kijisehemu cha maandishi ndani ya Katiba!

Haya ndiyo maoni ya Dkt Evans Makhulo – mshairi shupavu, msomi wa fasihi, mlezi wa vipaji na mjasiriamali anayeinukia vyema katika uandishi wa vitabu vya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Makhulo alizaliwa mnamo 1986 katika kijiji cha Itete, eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw Sylvester Makhulo na Bi Lilian Apondi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Itete kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Nanyeni, Matungu akiwa mwanafunzi wa darasa la nne. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 2002.

Makhulo alisomea katika Shule ya Upili ya Koyonzo, Kakamega kuanzia mwaka wa 2003. Alifanya Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2006 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kwa shahada ya ualimu (Kiswahili na Historia) mnamo 2008.

Alifaulu vyema kwa kupata daraja ya juu (First Class) mnamo 2012 na ufanisi huo ukampa ufadhili wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia 2013.

Alifuzu mnamo 2015 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Mamlaka na Itikadi katika Nyimbo Teule za Taraab” chini ya usimamizi na uelekezi wa Prof Rayya Timammy na Dkt James Zaja Omboga.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kwa minajili ya shahada ya uzamifu (phD) mnamo 2016. Alifuzu katika mwaka wa 2019 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Ukosefu wa Upole katika Matini ya Nyimbo za Taarab”.

Makhulo anatambua ukubwa wa mchango wa walimu wake wa awali katika kumhimiza kukichapukia Kiswahili. Baadhi yao ni Bw Joseph Mugera na Bw William Nyangweso waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Koyonzo.

“Nilitamani sana ije siku ambapo nami ningekuwa na umilisi mkubwa wa lugha, nikisarifu Kiswahili kama walivyokuwa wakizungumza walimu hawa kwa mvuto, ucheshi na ujasiri. Ama kweli, kinolewacho hupata!”

Wengine waliompokeza malezi bora ya kiakademia katika Chuo Kikuu cha Nairobi ni Prof Kyallo Wadi Wamitilia na Prof John Habwe. Hawa ndio walimwamshia Makhulo ari ya kukipenda Kiswahili tangu walipokuwa waendeshaji wa kipindi ‘Lugha Yetu’ katika Shirika la Habari la Kenya (KBC).

Makhulo anaamini kuwa Kiswahili kina uwezo wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ujuzi, ajira na uvumbuzi.

UALIMU

Makhulo alijitosa katika ulingo wa ualimu mnamo 2012. Alifundisha katika Shule ya Upili ya Koyonzo kwa muda mfupi kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya St Teresa’s Eastleigh, Nairobi mnamo 2014.

Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi. Amewahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya St Francis Rang’ala Girls, Kaunti ya Siaya mnamo 2016. Janga la corona lilimzimia ndoto ya kutua Amerika kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha St Lawrence, New York mwanzoni mwa mwaka wa 2020.

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Makhulo tangu utotoni. Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na upili, nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake na akawa maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Ilhamu anayojivunia katika ulingo wa uandishi ilichangiwa zaidi na walimu waliotambua mapema utajiri wa kipaji chake katika utunzi wa kazi bunilizi.

Uandishi wa Makhulo umeathiriwa pakubwa na kazi za Profesa Kithaka wa Mberia na Prof Abdilatif Abdalla – washairi shupavu, wasomi maarufu na mikota wa lugha wanaozidi kumpa ari ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili.

Kufikia sasa, Makhulo anajivunia kuandika na kuchapishiwa makala kadhaa ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Ametunga hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika mikusanyiko mbalimbali. Amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia Na Mashairi Mengine’ na ‘Malenga wa Afrika’ zilizochapishwa na African Ink Publishers mnamo 2021. Baadhi ya tungo zake huchapishwa mara kwa mara katika gazeti hili la ‘Taifa Leo’.

Baada ya kuchangia uhakiki wa ‘Kamusi Elezi ya Kiswahili’ iliyotolewa na Jomo Kenyatta Foundation (JKF) mnamo 2017, Makhulo aliandika ‘Mwongozo wa Kigogo’ uliofyatuliwa na Phoenix Publishers mnamo 2019.

Baadhi ya hadithi zake ni ‘Siwezi Tena katika mkusanyiko wa ‘Siwezi Tena na Hadithi Nyingine’ (Chania Publishers), ‘Mwisho wa Mwisho’ katika diwani ya ‘Mwisho wa Mwisho na Hadithi Nyingine’ (Mentor Publishers) na ‘Mke wa Jirani’ katika mkusanyiko wa ‘Mkaguzi wa Shule’ uliochapishwa na Education Distinction Publishers mnamo 2021.

Makhulo ameandika pia miswada mingi ya riwaya na tamthilia ambayo sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu.

JIVUNIO

Ndoto ya Makhulo ni kufikia upeo wa taaluma yake na kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi aliowafundisha katika ngazi na viwango tofauti vya elimu. Mmoja wao ni mwanahabari wa KU-TV, Bw Kevin Okello.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Makhulo ni kupanua wigo wake wa ujasiriamali, kufyatua diwani itakayobadilisha sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Ushairi wa Kiswahili na kuwalea waandishi chipukizi wa kazi za kibunifu.

Zaidi ya kuhudhuria makongamano mengi ya kupigia chapuo Kiswahili, Makhulo amekuwa akichangia mijadala ya kitaaluma na kuchanganua masuala ya siasa kupitia runinga mbalimbali nchini Kenya.

You can share this post!

WALLAH BIN WALLAH: Tumia Kiswahili kujinyanyua kimaisha,...

Wilbaro ya Ruto imeshika kutu, Kieleweke wadai