• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
HARAMBEE STARS: Mulee atakiwa atembelee kujionea vipaji Pwani

HARAMBEE STARS: Mulee atakiwa atembelee kujionea vipaji Pwani

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

WASHIKA dau wa soka kutoka sehemu mbalimbali za jimbo la Pwani jana walimtaka kocha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Jacob “Ghost” Mulee afike mwenyewe huko kushuhudia wachezaji wenye vipaji ambao wataweza kumvutia kuwaweka kikosini.

Kocha Mohamed Dadi wa Skyward Express FC ya Lamu amesema bila shaka Mulee amejionea mwenyewe wanasoka wawili wa Bandari FC, Danson Namasaka na Abdalla Hassan walivyomtosheleza kwa jinsi walivyocheza mechi dhidi ya Sudan Kusini na Tanzania.

“Nina imani kubwa kuwa mkufunzi wetu huyo ametosheka na jinsi wachezaji wetu hao wawili walivyokipiga na ningemuomba atokee huku mwenyewe kujiuonea kwani kuna wengi wanaoweza kumpendeza na kuwaingiza katika kikosi chake,” akasema Dadi.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally amesema alitambua kuwa Hassan na Namasaka wataweza kufanya vizuri kwenye timu ya taifa na akampongeza Mulee kwa kuwapa fursa wanasoka hao wawili kucheza na kuhakikisha uzuri wa uchezaji wao.

“Tuna wanasoka wengi wa Bandari ambao wanafaa kuwa katika kikosi cha Stars wakiwemo kina Bernard Odhiambo, Brian Otieno, Mohamed Siraj na Darius Msagha, nataraji nao watajaribiwa siku za usoni,” akasema Baghazally.

Meneja wa Bandari FC Albert Ogari alimpongeza kiungo wake Danson Namasaka kwa jinsi alivyocheza vizuri kwenye mechi ya Harambee Stars ilipokutana na Sudan Kusini siku ya Jumamosi iliyopita.

Ogari alimpongeza mchezaji huyo kwa alivyofanya vizuri katika pambano hilo ambapo yeye ndiye aliyetoa pasi iliyosababisha bao la ushindi la Stars. “Nilifurahikia na jinsi Namasaka alivyokipiga pamoja na Abdalla Hassan na nina imani kubwa wanasoka wetu wengine watamvutia mkufunzi huyo.

Alisema ana imani kubwa Hassan na Namasaka watakuwa miongoni mwa wale watakaokuwa katika kikosi cha Harambee Stars kitakachokabiliana na Misri na Togo kwenye mechi za Kanda G za kufuzu kwa fainali za Afcon.

Ogari anaamini kuwa Mulee atakuwa akiwaangazia wachezaji wazuri na kuwapa nafasi ili wapate kuonyesha ubora wao hasa jkwenye mechi za majaribio. “Nina imani kubwa Bandari tuna material za kuchezea timu ya taifa wakipewa nafasi,” akasema.

You can share this post!

Uhuru amwomboleza mwanahabari aliyefariki kutokana na corona

Vyakula hivi si vya kuliwa kila mara