• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Serikali yaonya wanaopandisha nauli kiholela

Serikali yaonya wanaopandisha nauli kiholela

NA RICHARD MAOSI

MSHIRIKISHI wa Bonde la Ufa George Natembeya ametoa onyo kali kwa sekta ya matatu , dhidi ya kuongeza nauli kiholela, tangu Rais Uhuru Kenyatta atoe agizo la kufunga kaunti za Kiambu, Machakos, Kajiado, Nakuru na Nairobi wiki iliyopita.

Wasafiri wengi walipigwa na mshangao kuanzia Jumamosi, baada ya kufika stejini na kupata nauli , zikiwa zimeongezeka kati ya asilimia 200 na 300.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Natembeya alisema baadhi ya wamiliki wa matatu za usafiri wa umma(PSV) walikuwa wakitumia fursa hiyo kuwanyanyasa wasafiri kwa kutoza nauli ya juu.

“Imekuwa ni desturi kila mara serikali inapotoa utaratibu wa kukinga raia dhidi ya maambukizi ya corona, wamiliki wa matatu kwa upande mwingine wanatumia fursa hiyo kukamua pesa kutoka kwa abiria,”akasema.

Alisema kuwa tabia hiyo haitaruhusiwa, na serikali iko tayari kupambana na wale wanaofikiri watatumia njia ya mkato kutengeneza hela..

Siku ya Jumamosi nauli kutoka Nakuru hadi Nairobi ilikuwa ni baina ya 2000-2500 huku baadhi ya wasafiri wakiahirisha safari.

Hali ilikuwa kama hiyo kutoka Nairobi mpaka Eldoret ambapo matatu nyingi zilitoza kati ya 3000 na 3500.

Aidha Taifa Leo Dijitali ilishuhudia msongamano mkubwa wa wasafiri kwenye steji ya Railways na ile ya Kingdom Seekers ambapo wasafiri wengi walikwama.

Msongamano wa magari kwenye steji ya Railways Nakuru, siku ya Jumapili. Wengi wao ni wanafunzi na wanalia bei ya nauli ilikuwa imepanda kwa asilimia 300. Picha/Richard Maosi

Kati ya walioadhirika ni wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za kiufundi ambao walikuwa mbioni kurudi nyumbani siku ya Jumapili, kabla marufuku ya kutosafiri baina ya kaunti hizi tano kutekelezwa rasmi.

Mmoja wao ni Caleb Ombui ambaye ni mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu Cha Embu ambaye anasema alikuwa ameishiwa na nauli baada ya kutumia 1700 kutoka Nairobi mpaka Nakuru.

Ombui ambaye alikuwa akielekea kaunti ya Transnzoia anasema kufikia mwendo wa saa kumi na mja jioni magari yote ya Kangaroo Shuttle yalikuwa yamejaa.

Isitoshe alilazimika kulipa 2000 zaidi kabla ya kufika nyumbani, isipokuwa magari yote yalikuwa yamejaa.

“Tunaomba serikali iingilie kati ili kudhibiti nauli hususan kwa wanafunzi ambao ndio wanahangaika zaidi,”akasema.

Baadhi ya madereva ambao hawakutaka kutajwa wanasema bei ya mafuta ndio chanzo ya kuongezeka kwa nauli.

 

You can share this post!

Taharuki watu watatu wakiuawa Kenol

Afueni kwa wakazi wa Machakos Gavana Mutua akiwapunguzia...