• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Hii ni aibu! Kocha Arteta achemka baada ya kichapo cha Liverpool

Hii ni aibu! Kocha Arteta achemka baada ya kichapo cha Liverpool

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal alisema “haikubaliki kabisa” mchezo ambao timu yake ilionyesha ilipolimwa magoli 3-0 na Liverpool uwanjani Emirates mnamo Jumamosi.

Arsenal kwa sasa wamejizolea alama 42 pekee katika mechi 30 zilizopita za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Pengo la pointi tisa linatamalaki kati yao na nambari nne Chelsea, ambao ni miongoni mwa vikosi vinavyowania fursa ya kukamilisha ligi ndani ya mduara wa nne-bora, na hivyo kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

“Liverpool walituzidi ujanja katika kila idara. Walijituma vilivyo na kucheza kwa makini. Walitulemea. Ni mimi nastahili kulaumiwa kwa matokeo hayo mabovu.

“Tungependa kuwaomba mashabiki na klabu nzima msamaha,” akatanguliza Arteta.

Ilivyo, nafasi ya pekee kwa Arsenal kufuzu UEFA msimu ujao ni kubeba taji la Uropa muhula huu.

Masogora hao wa Arteta watakuwa wenyeji wa Slavia Prague katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali za Uropa Ligi mnamo Alhamisi, kabla kurudiana ugenini nchini Czech wiki moja baadaye.

Arteta amewataka vijana wake kujinyanyua haraka baada ya kuaibishwa na Liverpool.

“Bado ningali katika mshangao, sikutarajia matokeo hayo. Hakika hatuwezi tena kushuka chini kiasi hicho,” alieleza Mhispania huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Arsenal.

“Haya ni matokeo yasiyokubalika kabisa kwa watu wanaowakilisha Arsenal na wanaopenda klabu hii. Lazima wachezaji wajifufue haraka.”

Arsenal wakidorora Liverpool waliweka hai matumaini ya kumaliza ligi ndani ya nne-bora.

Sasa ni alama mbili pekee lipo kati ya mabingwa hao watetezi na Chelsea, waliokubali kichapo cha 5-2 kutoka kwa West Bromwich Albion ugani Stamford Bridge siku ya Jumamosi.

Kila kikosi EPL kimesalia na takriban mechi nane za kusakata muhula huu.

 

You can share this post!

Inter Milan yaanza kunusia taji la Serie A

Jinsi sheria inavyoweza kuliweka taifa katika giza kipindi...