• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jinsi sheria inavyoweza kuliweka taifa katika giza kipindi cha janga la Covid-19

Jinsi sheria inavyoweza kuliweka taifa katika giza kipindi cha janga la Covid-19

Na MWANGI MUIRURI

SHERIA kuhusu uchapishaji habari hata kwa mitandao ya kijamii nchini Tanzania ni njia moja ambayo itaishia kuwanyima watafiti fursa ya kupata data kuhusu hali halisi kuhusu ugonjwa wa Covid-19.

Taifa hili likiwa tayari limekataa kutambua uwepo wa virusi hivyo katika mipaka yake, sheria hiyo ya Electronic and Postal Communications (Online Content) huzima uchapishaji wa aina yoyote kuhusu magonjwa hatari na maambukizi nchini humo au kwingineko bila ruhusa ya Serikali.

Ni sheria ambayo hata huenda iwanyime wenyeji Tanzania habari kuhusu jinsi mataifa mengine yanavyochukulia janga hilo la corona.

Ni hali ambayo imesumbua vitengo husika vya afya chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) haswa ikifahamika kuwa taifa hilo hata limekataa kupokezwa chanjo za COVID-19.

Hayo yakiendelea, Rais mpya Bi Suluhu Hassan hajaonyesha nia yoyote ya kubatilisha msimamo wa mtangulizi wake Rais John Pombe Magufuli wa kusisitiza Tanzania hakuna “coronavirus wala Covid-19. Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021, alizikwa Machi 26, 2021.

Kwa mfano, katika mazishi ya Magufuli nyumbani Chato, kuliibuka uwezekano kuwa taifa hilo haliko tayari kutambua maradhi hayo.

Huku ulimwengu mzima ukisisitiza umuhimu wa kuvaa maski kama njia moja ya kuzima uenezaji wa virusi hivyo katika umati, asilimia kubwa ya Watanzania waliojitokeza katika mazishi hayo hawakuwa na hizo maski na hata hakuna tahadhari iliyotekelezwa ya kukaa umbali wa mita mbili kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine.

Aidha, hakukuwa na ile tahadhari ya kupima joto la waombolezaji waliofika katika maziko hayo, hakukuwa na watu kunawa mikono kwa wingi wao wala sanitaiza kunyubyuzia kwa maikrofoni …. Maisha ni kawaida tu Tanzania, ikaibuka.

Wakenya waliokuwa wakifuatulia mazishi hayo yaliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga za kitaifa Ni lazima wengi walikuwa hawaamini macho yao ikizingatiwa kwamba Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imefanikiwa pakubwa kuogofya watu na jumbe za kuangazia ugonjwa wa Covid-19 kama bodaboda ya mauti yenye ukiabiri, steji ya kwanza ni kaburini.

Hata Serikali Kenya imetunga sheria za kuadhibu wasiovaa barakoa hadharani, hukumu ikiwa ni faini ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita korokoroni au zote mbili.

Alipoaga dunia Dkt Magufuli akiwa na umri wa miaka 61, licha ya kuweko kwa uvumi kwamba aliugua Covid-19, taarifa rasmi ya serikali ya Tanzania iliyosomwa na Mama Suluhu kabla ya avune cheo cha urais kutokana na msiba huo, ilisema kuwa mwendazake alifariki kutokana na maradhi ya moyo.

Baada ya Bi Suluhu kuapishwa kuwa Rais wa Sita na kuendeleza awamu ya Magufuli iliyotamatika baada ya kuwa kwa usukani kwa miaka sita, ilitarajiwa kuwa huyu Mama shujaa angetambua kuweko kwa virusi vya corona na angekuwa suluhu kwa kero ya Covid-19 sawa na jina lake.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus akimpa kongole zake Bi Suluhu kwa kuapishwa kuwa rais alisema kuwa “ni matumaini yangu sasa kuwa tutashirikiana kupambana na Covid-19.”

Taifa hili la Afrika Mashariki halijachapisha data kuhusu Covid-19 katika taifa hilo tangu Mei 2020 na hata limedinda kujihusisha na chanjo zinazosemwa kuwa na uwezo wa kukinga maambukizi ya maradhi haya.

“Ni matumaini yangu kuwa sasa tutashirikiana ili kuwakomboa Watanzania kutokana na maradhi haya ya Covid-19 ndio tuwe na afya bora ya Watanzania tukiangamiza maradhi ya kila aina hasa haya ya sasa ya kuletwa na virusi vya Corona,” akasema Dkt Ghebreyesus.

Hata hivyo, Bi Suluhu hajajibu mwito huo, hajatambua kitaifa kwa njia rasmi kuwa Covid-19 ni maradhi yanayotishia maisha ya Watanzania na hajatoa ishara yoyote ya kutambua ugonjwa huu kama kero kwa watu wake.

La mno, Rais huyo mpya wa Sita sasa aliongoza Watanzania kujitokeza kwa maziko ya mwendazake akiwa hana maski, kumaanisha ni sera rasmi kuwa Covid-19 ni hekaya tu nyingine ya Abunuwasi—mwenye macho akiambiwa haambiwi tazama.

Hata hivyo, kulikuwa nao ndani ya umati huo ambao walionekana kutambua Covid-19 iko na wakawa wamevalia barakoa zao, mfano ukiwa Rais wa Nne wa taifa hilo, Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Magufuli alikuwa ametangaza sera rasmi kuwa “hapa Tanzania hakuna Covid-19 na ikiwa utajipata na dalili sawa na zinazosemwa kuwa ishara za ugonjwa huo, mtumie mbinu za kienyeji na mumtegemee Mwenyezi Mungu katika maombi ya uponyaji.”

Alikataa katakata kufunga uchumi wa taifa hilo, akaendeleza kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na akawa kiongozi wa kusema na kutenda—akisema hakuna Covid-19 akaongoza kwa kukataa katakata kuutambua kisera.

Kwa wakati mmoja alinukuliwa akisema: “Hatuvai maski… Na hatutazivaa. Unafikiria ni kwa sababu hatuogopi kufa? La! Ni kwa sababu hakuna Covid-19.”

Baadaye alibadili msimamo akisema kuwa “ndio kuna ugonjwa ambao umezuka na ambao unawafanya waathiriwa wakumbwe na shida za kupumua” lakini hakutambua ulikuwa ni Covid-19 licha ya wachungaji kukiri walikuwa wameathirika.

  • Tags

You can share this post!

Hii ni aibu! Kocha Arteta achemka baada ya kichapo cha...

Hospitali mpya zimehudumia wagonjwa 16,000 jijini –...