Ajali ya mabasi mawili Kwa Shume yasababisha vifo vya si chini ya watu 14

CHARLES LWANGA na SAMMY WAWERU

WATU si chini ya 14 wamefariki baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya katika barabara kuu ya Malindi-Mombasa, iliyotokea Jumatano asubuhi.

Ajali hiyo katika eneo la Kwa Shume karibu na Kizingo, Kaunti ya Kilifi, ilihusisha basi la kampuni ya usafiri na uchukuzi ya Muhsin na basi la Sabaki T Shuttle.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kutwa Olaka na aliyezuru eneo la mkasa, alisema basi la Muhsin lilikuwa likielekea Garsen kutoka Mombasa, huku lile la Sabaki T Shuttle likielekea Mombasa kutoka Malindi.

Aidha, ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa moja asubuhi.

Abiria 18 walipata majeraha mabaya, na wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

“Tumelaza watu 18 ambapo sita kati yao wako katika hali mahututi,” akasema mkuu wa Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, Dkt Joab Gayo.

Alisema kati ya 18 hao, 14 ni wa jinsia ya kiume na wanne ni wa jinsia ya kike.

Wengine waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya Tawfiq na Star, zote zikiwa za wamiliki binafsi, mjini Malindi kupokea matibabu.

Madereva wa mabasi hayo walifariki papo hapo.

Mojawapo ya mabasi hayo lilikuwa na wafanyakazi kadha wa serikali ya Kaunti ya Kilifi.

Miili ya walioangamia ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi.

Habari zinazohusiana na hii