• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kenya sasa yaanza kujitengenezea silaha

Kenya sasa yaanza kujitengenezea silaha

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta jana alizindua kiwanda cha kutengeneza bunduki katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Rais alisema kiwanda hicho kitakuwa kikitengeneza bunduki ndogo, lakini kitapanua shughuli zake kwa kutengeneza bunduki kubwa na za kisasa katika muda wa miaka mitano ijayo.

Alisema kuwa tayari, kiwanda hicho kiMEtengeneza bunduki 12,000.

Rais alisema kuwa Kenya ilijiunga na nchi zinazotengeneza bunduki ili kupunguza gharama zinazotumika kununua silaha hizo.

“Lengo letu ni kuipa sekta ya usalama nchini uhuru katika utendakazi wake,” akasema.

Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kununua silaha kama vile bunduki ambazo hutumika na vikosi vya usalama.

Baadhi ya nchi ambazo huiuzia Kenya silaha hizo ni Uingereza, Urusi na Amerika.

Kando na bunduki, Kenya hutumia mabilioni ya fedha kila mwaka kununua vifaa vingine vya usalama kama vile ndege za kivita kwa operesheni za kijeshi na taasisi zingine za usalama.

Mpango huo pia unaonekana kutatua malalamishi ya baadhi ya vikosi vya usalama, hasa polisi, kuhusu uhaba wa silaha za kutosha kuwawezesha kuendesha operesheni zao za kudumisha usalama.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta alieleza imani yake kuwa kupitia kiwanda hicho, Kenya itapanua shughuli zake kwa kiwango cha kuanza kuyauzia silaha mataifa mengine katika ukanda huu.

Kando na kiwanda hicho, alieleza kuna mipango ya kubuni kiwanda kingine mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Janga la virusi vya corona limetufunza kuwa huenda mfumo wa kununua silaha kutoka nchi za nje ukaathiriwa na mambo mbalimbali yanayoendelea duniani,” akasema.

Alieleza kuwa thuluthi mbili ya vifaa vilivyotumika kutengenezea silaha hizo zimetolewa hapa nchini.

Alisema kuwa awali, kiwanda hicho kilipangiwa kuigharimu serikali Sh15 bilioni, lakini kiwango hicho kikapungua kwa karibu robo ya fedha hizo baada ya utathmini mpya kufanywa.

“Ni imani yangu kuwa katika muda wa miaka mitano ijayo, Kenya itakuwa na uwezo wa kutoa silaha za ulinzi wa taasisi zote za usalama,” akasema.

You can share this post!

UHURUTO WALIVYOFUTA REKODI YA KIBAKI

Raila amtumia Ruto ujumbe wa muungano