• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Madaktari walioenda Cuba warejea Kenya kuanza kazi

Madaktari walioenda Cuba warejea Kenya kuanza kazi

Na MARY WAMBUI

MADAKTARI 48 raia wa Kenya waliotumwa nchini Cuba na Wizara ya Afya kwa masomo ya uzamili kuhusu Tiba ya Jamii sasa wamerejea nchini kwa awamu ya mwisho ya masomo yao.

Watatumwa katika vituo mbalimbali katika kaunti zote 47 kwa kipindi cha miezi tisa ijayo kuanzia juma hili.Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Martin Wambora alifichua hayo jana alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mikakati inayotekelezwa na kaunti kukabiliana na janga la Covid-19.

“Kama baraza, tunashukuru Wizara ya Afya kwa kuwezesha mafunzo maalum kwa madaktari, ambayo yatachangia pakubwa kuimarisha mifumo yetu ya afya,” alisema Gavana Wambora.

Pindi tu watakapokamilisha masomo yao, madaktari hao wataungana na juhudi za madaktari wengine 53 wa jamii kutoka Cuba, waliokuja nchini mnamo 2018, kuziba pengo muhimu nchini kuhusu utowaji wa huduma maalum.

Mafunzo na taaluma ya madaktari wa jamii yanatilia maanani zaidi kuzuia maradhi na kuimarisha afya.Inatarajiwa kuwa kazi yao itasaidia kupunguza mzigo wa maradhi yanayoweza kuzuiwa ili matabibu wengine watilie maanani huduma za afya kuhusu tiba, jinsi inavyohitajika.

Kwa sasa, taifa linakabiliana na janga la Covid-19. COG ilionya kuwa, kunaibuka mkondo wa kutisha ambapo watu waliopokea chanjo wanakosa kufuata kanuni kutokana na dhana ya kupotosha kwamba chanjo ni hakikisho ya kuwa na kinga ya mwili dhidi ya virusi hivyo.

Katika majuma ya hivi punde, kaunti za Nakuru, Kakamega, Meru, Uasin Gishu, Murang’a, Nyeri na Kisumu zimeripoti kuongezeka kwa idadi ya maambukizi.COG imeonya kwamba hali hiyo huenda ikalemea mifumo ya afya katika kaunti husika endapo itaendelea.

“Ili kuepuka hali ya kulemazwa kwa sera, ambayo imeshuhudiwa katika mataifa mengine, serikali zote za kaunti 47 zitatoa ripoti kuhusu idadi ya visa, hatua zilizochukuliwa, udhaifu na mikakati iliyowekwa,” alisema Bw Wambora.

Aidha, serikali za kaunti kwa ushirikiano na serikali kuu kupitia Kamati za Serikali za Kaunti, zitafanya majaribio ili kujiandaa kwa uwezekano wa kuzuka kwa hali mbaya zaidi ili kaunti ziwe tayari kwa jambo lolote.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, idadi ya jumla ya vitanda vya wagonjwa waliotengwa katika kaunti, imeongezeka hadi 6,253 baada ya wagonjwa 50 kupona.

You can share this post!

ODM yawaagiza wabunge wake waipitishe BBI

Korti yamzima Orengo kuwa wakili wa Manduku