• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
IEBC yataka waliochochea vurugu Juja wachukuliwe hatua kali kisheria

IEBC yataka waliochochea vurugu Juja wachukuliwe hatua kali kisheria

Na SAMMY WAWERU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inataka waliochochea vurugu wakati wa shughuli ya kuhesabu kura eneobunge la Juja, Jumanne usiku, kuchukuliwa hatua kali kisheria.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Jumatano ameihimiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kufanya uchunguzi na kuwashtaki waliohusika.

Jumanne, wapigakura wa Juja walishiriki uchaguzi mdogo kuchagua mbunge wao baada ya kiti hicho kusalia wazi kufuatia kifo cha Bw Francis Munyua Waititu maarufu kama Wakapee, mnamo Februari 2021.

Wakati kura zikijumuishwa, kundi la vijana linalodaiwa kuongozwa na Gavana wa Kiambu James Nyoro, kwa mujibu wa taarifa ya IEBC, lilivamia baadhi ya vituo vya kuhesabu kura.

“Visa tulivyoshuhudia vilikuwa katika vituo vinne vya kuhesabu kura. Maafisa wetu hata hivyo walikuwa wamemaliza kuhesabu,” amesema Bw Chebukati.

Huku IEBC ikiweka zingatio kwenye matukio na visa vya Jumanne, Chebukati amesema atamwandikia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji barua kuchunguza waliochochea vurugu.

“Tukiendelea kusubiri matokeo ya uchunguzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), tutamwandikia barua DPP kufanya uchunguzi zaidi na kuchukulia hatua kali wahusika,” akasema.

You can share this post!

Leeds United wazamisha chombo cha Southampton

Masogora tisa wanaopiga soka ya EPL waitwa kambini mwa timu...