Corona imeua wengi zaidi kinyume na taarifa – WHO

Na MASHIRIKA

GENEVA, Uswisi

JUMLA ya watu 1.2 milioni duniani walifariki kutokana na makali ya Covid-19 bila kuambukizwa na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo kufikia Desemba 31, 2020, ripoti mpya imebaini.

Hii ni kando na watu 1.8 milioni waliokufa baada ya kuambukizwa na ugonjwa huo, kulingana na takwimu ambazo nchi mbalimbali ziliwasilisha kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) wakati huo.

Kwa hivyo, inakadiriwa kuwa angalau watu milioni tatu (3 milioni) walifariki kutokana na corona, pamoja na madhara mengine yanayosababishwa na janga hilo, kama vile njaa na msongo wa mawazo.

Huku idadi ya hivi punde ya vifo vya corona iliyoripotiwa kwa WHO ikizidi watu 3.3 milioni, huenda nchi mbali mbali zinatoa idadi ya chini ya vifo vya moja kwa moja na vinavyosababishwa na madhara mengine ya Covid-19.

“Huenda watu wengi wanafariki kutokana na Covid-19 kuliko inavyoripotiwa na nchi mbalimbali za ulimwengu. Isitoshe, kuna watu ambao wanafariki kutokana na corona bila kupimwa kubaini ikiwa wana virusi na wengine wanaofariki kutokana na makali au madhara yanayosababishwa na janga hili,” ikasema WHO katika ripoti yake ya uchunguzi, “Pulse Survey” iliyotolewa Ijumaa.

Kulingana na WHO, baadhi ya nchi zinaripoti vifo vya wagonjwa wa Covid-19 vinavyotokea hospitalini pekee au vifo vya watu waliopimwa na kupatikana na virusi vya corona.

“Vile vile, nchi nyingi hazina uwezo wa kukadiria au kuripoti chanzo cha vifo kutokana na changamoto zinazokumba taasisi za kiafya kama vile uhaba wa vifaa na wataalamu wenye ujuzi,” inaongeza ripoti ya utafiti ulioendeshwa katika nchi 135 kote ulimwenguni Machi, 2021.

“Sharti nchi zote zijizatiti kupata uwezo na vifaa hitajika kukusanya data sahihi na kuzitumia hata wakati kama huu wa janga la Covid-19,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.

“Mlipuko wa janga hili umeonyesha kuwa ipo haja ya ukusanyaji wa data sahihi ili kujenga mifumo ya kulidhibiti sawa na maradhi mengine,” akaongeza.

WHO inasema, katika ripoti hiyo, kwamba, huenda janga la Covid-19 limechangia ongezeko la vifo kutokana na changamoto zinginezo, kama vile kuvurugwa kwa taratibu za utoaji huduma za afya na utoaji chanjo dhidi ya maradhi mengine.

Aidha, idadi ya watu wanaosaka huduma za matibabu katika vituo vya afya imepungua sawa na kupungua kwa ufadhili wa mpango wa kupambana na maradhi mengine kama vile malaria na kansa.

Kulingana na WHO, asilimia 90 ya nchi zilizoshirikishwa katika uchunguzi wake zilipatikana kuathirika na changomoto zilizoathiri mfumo wa utoaji huduma za afya.

Habari zinazohusiana na hii

Dkt Mogusu atawagusa?