• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
TAHARIRI: NHIF ifae maskini wanaougua corona

TAHARIRI: NHIF ifae maskini wanaougua corona

KITENGO CHA UHARIRI

TANGAZO la mwenyekiti wa Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) Bw Lewis Nguyai kwamba hazina hiyo haitagharimia matibabu ya Covid-19 kwa watu wasiolipia ada ya zaidi ya Sh1,000 kila mwezi linashtua na limevunja moyo Wakenya wengi.

Akali kubwa ya jumla ya Wakenya wapatao 8.4 milioni ambao ni wanachama wa hazina ya NHIF ni maskini. Hawa ndio hulipa ada ya Sh500 kila mwezi wakiwa na tumaini kwamba wakati watakapojipata katika ulazima wa kulazwa hospitalini, gharama ya matibabu itagharimiwa na hazina hii kwani ni bima ya Afya.

Hata hivyo, tangazo la mwenyekiti wa hazina ya NHIF lina maana kwamba ni wafanyakazi wa umma, wafanyakazi wa kaunti pamoja na watu wenye hali zao katika pekee ambao hulipia ada ya zaidi ya Sh1,000 kila mwezi kwa hazina hii ndio watakaopata matibabu dhidi ya maradhi endapo wataambuklizwa Covid-19.

Ni muhimu kusisitiza kwamba hazina hii ya kitaifa hasa ilinuiwa kuwafaa maskini. Kuwatelekeza maskini wakati wa shida ni sawa na kuwaua. Ni taifa katili pekee ambalo linafaa kuchukua hatua kama hii kwa raia wake wenye mapato ya chini.

Kama taifa, tunafaa kuwa na wasiwasi hasa ikizingatiwa kwamba tangazo hili linajiri wakati ambapo dalili zipo za kulipuka kwa wimbi la nne la ugonjwa wa Covid-19 kutokana na msambao wa virusi vyenye asili ya India humu nchini.

Ikizingatiwa kwamba kwa wastani takwimu zinaonesha kuwa mgonjwa mmoja huhitaji kiwango cha Sh21,000 kwa siku kama gharama ya matibabu, ni maskini yupi atapona? Ni kwa mintarafu hii ambapo tunasihi NHIF izingatie upya uamuzi ambao imeamua kuchukua kwa sababu athari zake zitakuwa mbaya zaidi kwa mamilioni ya Wakenya wenye mapato ya chini.

Isisahaulike kwamba hawa Wakenya wenye mapato ya chini ambao ndio wengi vile vile ndio nguvu kazi ya taifa ambao huendesha uchumi. Katika mataifa yaliyoendelea, matajiri na wafanyakazi wa umma wenye mapato makubwa ndio hutozwa ada ya kugharimia matibabu ya watu katika tabaka hili.

Serikali inafaa kuingilia kati na kubatilisha hatua ya hazina ya kitaifa ya NHIF kuokoa kundi hili dhidi ya balaa inayowakodolea macho. Wakenya wenye mapato ya chini wana hawa sawa na wachangiaji ada wengine katika NHIF kupata haki ya huduma bora za afya kutoka kwa bima ya kitaifa ambayo haifai kuwa baguzi.

You can share this post!

Hasara, hofu ndovu wakivivamia vijiji

WARUI: Pendekezo la TSC huenda liibue changamoto kwa walimu