• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
WARUI: Pendekezo la TSC huenda liibue changamoto kwa walimu

WARUI: Pendekezo la TSC huenda liibue changamoto kwa walimu

Na WANTO WARUI

PENDEKEZO la Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini (TSC), kutaka mabadiliko kuhusiana na kozi wanazomea walimu, linazua maswali kadha.

Tangazo hilo pia limetolewa wakati usiofaa ambapo taifa linakabiliwa na uhaba wa kazi na athari za ugonjwa wa Covid-19.

Tume imependekeza kufutiliwa mbali kwa digrii ya Elimu na kuwataka wanaotaka kuwa walimu kusomea digrii yoyote ya masomo ya sanaa au sayansi na kisha kusomea diploma ya masuala ya ualimu kwa mwaka mmoja.

Licha ya hayo, serikali haijaweza kuwaajiri walimu wote ambao wamepata mafunzo ya ualimu ya P1 na wengi wao wangali wanatafuta kazi hadi sasa. Na je, tangazo hilo linanuia kubana zaidi nafasi za ajira kwa walimu au kuwasimamisha kazi baadhi yao?

Baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu, wameelezea hofu yao kuwa hatua hii huenda ikawa ni njama ya TSC kuwapunguza wafanyakazi wake kama ilivyopendekezwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuwa ni sharti serikali ipunguze idadi ya waajiriwa katika mashirika yake ili iweze kupewa mkopo wa Sh257 bilioni. Ikiidhinisha mkopo huo kwa Kenya, IMF ilisema kuwa kuna vyuo vikuu vitatu nchini ambavyo ni lazima vipunguze matumizi yake ya fedha kwa kuwa vinatumia pesa nyingi sana katika mishahara.

Huenda vyuo hivi ni Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenyatta na Moi kwani ndivyo vyenye wafanyakazi wengi zaidi kuliko vile vingine vya umma nchini. Chuo kikuu cha Nairobi hulipa mishahara ya takriban Sh8 bilioni, Kenyatta takriban 5 bilioni na Moi takriban Sh4 bilioni. Vyuo hivi vitatu vina wafanyakazi zaidi ya 10,000.

Aidha sekta ya elimu ni mojawapo ya zile zilizowaajiri wafanyakazi wengi zaidi nchini wakiwemo walimu. Kwa mtazamo huu, serikali ingependa kupunguza matumizi yake ya fedha katika sekta hii na huenda huu ndio mpango wa TSC. Kwa kuinua viwango vya masomo kwa walimu, kuna watu wengi ambao hawataweza kufikia viwango hivi na hivyo basi itakuwa muhali kwa yeyote anayenuia kuwa mwalimu kujifunga kibwebwe ili aweze kupata nafasi hii ya ajira.

Kuna uwezekano pia kuwa, maandalizi haya yanafanywa kulingana na mpango wa kuwezesha mtaala mpya wa CBC kufaulu. Huenda ni maandalizi ya walimu watakaofunza viwango vya shule za upili za Gredi za 7 hadi 9 na Gredi za 10 hadi 12. Ikiwa huu ndio mtazamo wa TSC, basi inahitaji kuweka wazi malengo yake na kutangazia wananchi sababu za hatua inazozichukua.

Kama TSC itasimama kidete na tangazo hili lake, basi ni sharti iwashirikishe washikadau katika mpango huu wote ili uweze kufaulu. Ikiwa haitafanya hivyo na kuleta mabadiliko kwa kifua, basi washirika wengine kama vile vyuo watakataa na kudhalilisha mpango wote huo wa kutoa mafunzo hayo.

You can share this post!

TAHARIRI: NHIF ifae maskini wanaougua corona

KAMAU: Mageuzi yaja kwa viongozi wasaliti na wenye ubinafsi