• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Waogeleaji Wakenya Rosafio na Muteti wanatusisimua na matokeo mazuri tunapoelekea Olimpiki

Waogeleaji Wakenya Rosafio na Muteti wanatusisimua na matokeo mazuri tunapoelekea Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Uogeleaji Kenya (KSF) limefurahishwa na waogeleaji Danilo Rosafio na Emily Muteti watakaowakilisha Kenya kwenye Olimpiki mjini Tokyo, Japan mnamo Julai 23 hadi Agosti 8.

Rosafio alishinda medali ya shaba katika kuogelea mita 100 freestyle na kuweka muda bora katika kuogelea mita 50 freestyle kwenye mashindano ya kimataifa ya Porto nchini Ureno yaliyofanyika Juni 5-6.

Katika mahojiano ya Jumatatu na kaimu rais wa KSF, Zack Musembi alieleza Taifa Leo, “Ni matokeo mazuri sana tunapoelekea Olimpiki. Ametuchangamsha kwa kuimarisha muda wake kwa sekunde mbili na pia kushinda medali.”

Rosafio alikamilisha mita 50 kwa sekunde 23.52 akiimarisha muda wake bora uliokuwa 23.71. Wareno Diogo Matos na Fernando Souza walimaliza katika nafasi mbili za kwanza kwa sekunde 22.93 na 23.50, mtawalia.

Katika mita 100, ambazo pia Matos na Souza walikamata nafasi mbili za kwanza kwa sekunde 50.31 na 51.15, Rosafio aliambulia nishani ya shaba kwa sekunde 52.22.

Rosafio ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza ambako pia amekuwa akifanyia mazoezi.

Muteti, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Grand Canyon nchini Amerika, pia amekuwa akiandikisha matokeo mazuri katika matayarisho yake ya Olimpiki. Anatarajiwa kuwa nchini Ufaransa mnamo Juni 15-16.

Wakenya hao walipata tiketi baada ya Shirikisho la Uogeleaji Duniani (FINA) kulegeza sheria za kufuzu kwa sababu ya changamoto zilizosababishwa na janga la virusi vya corona.

You can share this post!

Tuwei: Sifan ameweka rekodi ya dunia ya mbio za mita...

Mkimbizi Msafiri akimbia kilomita zaidi ya kilomita 500...