Wakulima wahimizwa kukumbatia kilimo cha maparachichi ya Hass, kina faida

 

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA nchini wamehimizwa kukumbatia kilimo cha maparachichi aina ya Hass kutokana na ushindani wayo katika masoko ya ughaibuni.

Kiwango cha uzalishaji Kenya ni cha chini kikilinganishwa na mataifa mengine ulimwenguni kama vile Israili, Chile, Uhispania, Mexico, Brazil, Peru, Columbia na Argentina.Katika Bara la Afrika, Afrika Kusini imepiku Kenya katika uzalishaji wa avocado za Hass.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Kilimo, uuzaji wa maparachichi ya Kenya nje ya nchi ni asilimia tano pekee.Naibu Meneja kitengo cha mazao mbichi ya shambani, katika kampuni ya Kakuzi PLC, Bw Jonathan Kipruto ameambia Taifa Leo haja ipo wakulima wakumbatie ukuzaji wa maparachichi kutokana na mahitaji ya matunda hayo katika masoko ya nje.

Licha ya Hass kuonekana kuwa na mvuto, Bw Kipruto amesema kiwango cha wakulima nchini hakikithi soko linalohitajika.Kakuzi PLC imetia saini mkataba wa makubaliano na zaidi ya wakulima 3, 500 wa Hass, kuwatafutia soko la mazao nje ya nchi.

Kipruto alisema bei ya Hass inaendelea kunoga, katika mauzo ya mwaka uliopita, tunda moja la Hass likikadiriwa kununuliwa kati ya Sh18 – 39.“Mwaka wa 2019 bei ilikuwa bora zaidi kuliko 2020,” Kipruto akasema.

Afisa huyo alihimiza Wakenya kukumbatia zao hilo la thamani, akisema litawasaidia kujiimarisha kimaisha na kimaendeleo.“Ninawahimiza watathmini ubora na mapato ya maparachichi ya Hass. Kule nje soko lina ushindani mkuu,” akasema.

Picha/ Sammy Waweru.
Maparachichi yakipakiwa katika kampuni ya Kakuzi PLC, iliyoko Kaunti ya Murang’a ili kuuzwa nje ya nchi.

Mwaka wa 2019, Kenya ilitia saini mkataba wa makubaliano na China, Kenya kuuza maparachichi yake nchini humo.Hass ni aina ya avokado zilizoimarishwa na zenye ladha ya kipekee, kutokana na virutubisho vyake.Kakuzi PLC imeweza kupata soko ya matunda hayo katika nchi za Bara Uropa, Ufaransa na Uhispania.