• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Brazil waanza vyema kampeni za Copa America kwa kucharaza Venezuela 3-0

Brazil waanza vyema kampeni za Copa America kwa kucharaza Venezuela 3-0

Na MASHIRIKA

WENYEJI Brazil walianza kutetea ubingwa wa Copa America mnamo Jumapili usiku kwa kuwakung’uta Venezuela 3-0 katika uwanja wa Nacional de Brasilia.

Beki Marcos Marquinhos Correa wa Paris Saint-Germain (PSG) walifungulia Brazil ukurasa wa mabao katika dakika ya 23 kabla ya fowadi Neymar Jr ambaye pia anachezea PSG kupachika wavuni bao la pili kupitia penalti ya dakika 64. Neymar alichangia goli la tatu ambalo Brazil walifungiwa na Gabriel Barbosa mwishoni mwa kipindi cha pili.

Brazil ambao ni mabingwa mara tisa wa Copa America walitia kapuni ufalme wa kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12 mnamo 2019.

Maandalizi ya Venezuela kwa ajili ya mechi hiyo yalivurugwa pakubwa na virusi vya corona ambavyo viliathiri wanasoka 12 na baadhi ya vinara wa benchi ya kiufundi. Washindani wengine wa Brazil na Venezuela katika Kundi A ni Colombia, Ecuador na Peru.

Colombia walipepeta Ecuador 1-0 katika mchuano wao wa ufunguzi; bao hilo la pekee likifumwa wavuni na Edwin Cardona mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Kabla ya goli hilo kuhesabiwa, refa wa katikati ya uwanja alilazimika kurejea teknolojia ya VAR iliyobatilisha maamuzi ya awali ya waamuzi.

Fowadi Richarlison Andrade wa Everton aliyemwajibisha pakubwa kipa Joel Graterol wa Venzuela, alishuhudia pia bao alilofungia Brazil katika kipindi cha kwanza likifutiliwa mbali kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Neymar aliyepoteza nafasi nyingi za wazi, alifunga goli lake la 67 ndani ya jezi za Brazil baada ya beki Yohan Cumana kumchezea visivyo Danilo Luiz da Silva ndani ya kijisanduku. Ufanisi huo wa Neymar ulimsogeza karibu na rekodi ya kitaifa ya mabao 77 inayoshikiliwa na nguli wa soka Edson Arantes do Nascimento almaarufu Pele.

Makala ya 47 ya Copa America yanafanyika Brazil mwaka huu baada ya kuahirishwa mnamo 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Samba Boys wa Brazil wanapigiwa upatu wa kutamalaki mechi zote za Kundi A na hatimaye kuhifadhi taji la Copa America walilolinyanyua mnamo 2019 wakiwa waandalizi wa kinyang’anyiro hicho.

Brazil walipokezwa idhini ya kuwa wenyeji wa Copa America mwaka huu baada ya maandamano ya raia dhidi ya serikali kuzuka nchini Colombia na maambukizi ya virusi vya corona kuzidi nchini Argentina.

Colombia na Argentina ndio waliokuwa wawe waandalizi wa pamoja wa fainali za Copa America mwaka huu na ingekuwa mara ya kwanza tangu 1916 kwa fainali hizo kuandaliwa na mataifa mawili.

Kabla ya Brazil kupokezwa uenyeji wa Copa America mwaka huu, kulishuhudiwa pingamizi nyingi zilizowasilishwa mahakamani na washikadau mbalimbali wakiwemo wanasoka Henrique Casemiro wa Real Madrid na Neymar.

Hata hivyo, majaji wa Mahakama ya Juu nchini Brazil walitupilia mbali maombi yaliyokuwa yamewasilishwa kortini kuzuia fainali za kipute hicho kuandaliwa nchini humo kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa malalamishi, ilihojiwa kwamba maelfu ya raia na wakazi wa Brazil walikuwa katika hatari ya kuambukizwa corona iwapo fainali za Copa America zitaandaliwa nchini humo. Hata hivyo, majaji walishikilia kwamba Katiba ya Brazil haina uwezo wa kushinikiza korti kutoa amri ya kusitishwa kwa maandalizi ya kivumbi hicho.

Badala yake, walitaka magavana na mameya wa miji mikuu kuhakikisha kwamba kanuni zote za kudhibiti maambukizi corona zinazingatiwa katika himaya zao.

Vikosi vinavyoshiriki Copa America vitakuwa vikifanyiwa vipimo vya corona kila baada ya saa 48 huku wachezaji na maafisa wa vikosi vyao wakinyimwa uhuru wa kutembea ovyo. Kivumbi cha Copa America kilichokuwa kifanyike mnamo 2020, kiliahirishwa kwa sababu ya corona ambayo imesababisha zaidi ya vifo 480,000 nchini Brazil.

Hadi walipokutana Jumapili usiku, Brazil waliwahi kushinda Venezuela 1-0 walipokutana mara ya mwisho mnamo Novemba 2020 katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Japo mechi dhidi ya Brazil iliwapa Venezuela jukwaa mwafaka la kujinyanyua baada ya kushinda mchuano mmoja pekee kati ya sita iliyopita, walitolewa kamasi huku wakikosa huduma za mshambuliaji wao tegemeo, Salomon Rondon anayeuguza jeraha.

Mapema mwezi huu, Venezuela walitia kapuni alama moja pekee kutokana na mechi mbili za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia baada ya kupepetwa 3-1 na Bolivia kisha kuambulia sare tasa dhidi ya Uruguay.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wenyeji watumai kuzima mzozo na wasimamizi wa ‘shamba...

Benteke atia saini mkataba mpya wa miaka miwili kambini mwa...