• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ufaransa wang’aria Ujerumani kwenye gozi kali la Euro

Ufaransa wang’aria Ujerumani kwenye gozi kali la Euro

Na MASHIRIKA

UFARANSA waliotawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 walifungua kampeni zao za Kundi F kwenye Euro kwa kupokeza Ujerumani walioibuka wafalme wa dunia mnamo 2014 kichapo cha 1-0 mnamo Jumanne usiku jijini Munich.

Bao la pekee katika mchuano huo lilifumwa wavuni na beki Mats Hummels aliyejifunga katika dakika ya 20 baada ya kubabatizwa na kombora lililoachiliwa na kiungo Lucas Hernandez.

Hummels ambaye ni beki mahiri wa Borussia Dortmund alirejeshwa kambini mwa Ujerumani kwa ajili ya kampeni za Euro mwaka huu licha ya kutemwa na kocha Joachim Loew kwenye kikosi cha miamba hao mnamo 2019.

Ufaransa ambao ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu wa kutwaa taji la Euro, walianza kipindi cha kwanza kwa matao ya juu kabla ya kulemewa na Ujerumani katika kipindi cha pili baada ya mafowadi Timo Werner na Leroy Sane kuletwa uwanjani.

Kiungo Paul Pogba alishirikiana vilivyo na mafowadi Kylian Mbappe, Antoine Griezmann na Karim Benzema waliotegemewa na kocha Didier Deschamps katika safu ya mbele ya kikosi cha Ufaransa.

Mshambuliaji Thomas Muller ambaye pia alirejeshwa na Loew kambini mwa Ujerumani baada ya kuwa nje kwa kipindi cha miaka miwili, alipoteza nafasi kadhaa za wazi alizoundiwa na viungo Ilkay Gundogan na Serge Gnabry wanaochezea Manchester City na Bayern Munich mtawalia.

Mabao mawili ambayo Ufaransa walifungiwa na Mbappe na Benzema katika kipindi cha pili yalikataliwa kwa madai kwamba wawili hao walicheka na nyavu za Ujerumani wakiwa wameotea.

Ufaransa kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi F baada ya mabingwa watetezi Ureno kuwafunga Hungary 3-0 katika mchuano mwingine wa ‘kundi hilo la kifo’.

Huku Ufaransa wakijivunia kutwaa taji la Euro mara tatu, Ujerumani wamewahi kutawazwa mabingwa mara mbili. Hata hivyo, Ujerumani wamenyanyua Kombe la Dunia mara nne huku Ufaransa wakitia taji hilo kibindoni mara mbili pekee.

Kati ya wanasoka wote 22 walioanza mechi kati ya Ujerumani na Ufaransa mnamo Jumanne usiku jijini Munich, ni watatu pekee ambao hawajawahi kuongoza vikosi vyao kutia kapuni ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Hao ni Presnel Kimpembe wa Paris Saint-Germain (PSG), Ousmane Dembele wa Barcelona na kipa Hugo Lloris wa Tottenham Hotspur.

Ufaransa wanashiriki fainali za Euro mwaka huu wakipania kuunganisha ubingwa wa kipute hicho na ufalme wa dunia – sawa na walivyofaulu kufanya miaka 21 iliyopita.

Chini ya kocha Didier Deschamps, Ufaransa walipigwa 1-0 na Ureno kwenye fainali ya Euro 2016 jijini Paris. Huku Deschamps akilenga kuepuka masaibu sawa na hayo, mkufunzi Loew ana kiu ya kuachia mashabiki wa Ujerumani ‘kitu cha kujivunia’ kabla ya kubanduka rasmi kambini mwao mnamo Julai na mikoba anayodhibiti sasa kutwaliwa na kocha wa zamani wa Bayern Munich, Hansi Flick.

Miaka 20 tangu aongoze Ufaransa kutwaa kombe la Euro mnamo 2000 akiwa mchezaji, Deschamps anapania kujizolea taji la pili akiwa mkufunzi baada ya kikosi chake kuibuka mabingwa wa dunia miaka mitatu iliyopita nchini Urusi.

Japo Ufaransa walipigwa 2-0 na Uturuki mnamo Juni 8, 2019 katika mojawapo ya mechi za kufuzu kwa fainali za Euro, kikosi hicho kwa sasa kinajivunia ufufuo mkubwa. Kilikomoa Wales na Bulgaria 3-0 kwenye michuano miwili iliyopita ya kirafiki na wameendeleza rekodi ya kutofungwa bao kutokana na michuano mitano mfululizo.

Tangu washiriki kipute cha Euro kwa mara ya kwanza mnamo 1960, Ufaransa wamepoteza mechi moja pekee ya ufunguzi kwenye fainali hizo; hiyo ikiwa miaka 61 iliyopita ambapo walipokezwa kichapo cha 5-4 kutoka kwa Yugoslavia. Kwa upande wao, mechi dhidi ya Ufaransa ilikuwa ya kwanza kwa Ujerumani kupoteza kwenye ufunguzi wa kipute cha Euro.

Iwapo Ufaransa watatia kibindoni ufalme wa Euro mwaka huu, basi ufanisi huo utamfanya Deschamps kuwa mtu wa kwanza kuwahi kunyanyua taji hilo na kombe la dunia akiwa mchezaji na kocha.

Tangu watinge fainali ya Euro 2008 ambapo walikung’utwa 1-0 na Uhispania, Ujerumani hawajawahi kupiga hatua zaidi kwenye kipute hicho. Walibanduliwa na Italia kwenye nusu-fainali za 2012 baada ya kupigwa 2-1 kabla ya Ufaransa kuwadengua kwenye hatua hiyo ya nne-bora mnamo 2016 kwa kichapo cha 2-0.

Ujerumani walijibwaga dhidi ya Ufaransa wakilenga kujinyanyua badaa ya Macedonia Kaskazini kuwapepeta 2-1 mnamo Machi 31 kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Miamba hao waliwahi kupondwa 6-0 na Uhispania kwenye gozi la UEFA Nations League mnamo Novemba 2020; hicho kikiwa kichapo kinono zaidi kwa Ujerumani kuwahi kupokezwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 80.

Benzema alikuwa akirejea katika timu ya taifa Ufaransa kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa takriban miaka sita.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 hakuwahi kuchezea Ufaransa tangu 2015 baada ya kudaiwa kushiriki tukio la utapeli lililomhusisha aliyekuwa mchezaji mwenzake kambini mwa Ufaransa, Mathieu Valbuena.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jumwa apuuza hitaji la digrii kwa uongozi wa kisiasa

Ureno waanza kutetea taji la Euro kwa kuadhibu Hungary na...