Viongozi walalamikia Rais kutojali Mlima Kenya

Na MARY WANGARI

VIONGOZI kutoka eneo la Mlima Kenya wameelezea wasiwasi kuhusu kile wanachotaja kama hali ya kutojali ya Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu maslahi ya eneo hilo ya siku za usoni baada ya hatamu yake kufika kikomo 2022.

Aidha, wanasiasa hao wamemshutumu rais kwa kuvuruga juhudi za kiongozi yoyote kutoka eneo la Kati, ambaye anaonyesha dalili za kutaka kumrithi.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, aliyekuwa mbunge wa Starehe, Askofu Margaret Wanjiru, alisema inavunja moyo kwamba Rais Kenyatta anapuuza Mlima Kenya – eneo ambalo ni ngome yake kuu kisiasa, iliyompigia kura kwa wingi katika chaguzi kuu za 2012 na 2017.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kugombea kiti cha ugavana Kaunti ya Nairobi, na ambaye bado ametangaza kuwania wadhifa huo kwa mara nyingine, alimshutumu rais kwa kuwanyamazisha viongozi wanaoonekana kuwa na nia ya kumrithi, badala ya kuwakuza.

“Kwa mtazamo wa Mlima Kenya, kama mtu anayetoka eneo hilo, tuna wasiwasi kwamba rais hatupi ishara za kutuacha katika mikono salama. Kama kiongozi unapaswa kupokeza usukani wa uongozi wako kwa mikono salama, ambayo inaweza kuwatunza watu,” alisema Bi Wanjiru.

Aliongeza: “Badala yake, anachofanya ni kutawanya viongozi wetu; yeyote anayeonekana kuwa na umaarufu eneo letu, anayeonekana kufanikiwa. Anawashambulia na kuwaangamiza, na hilo halifai.

“Kama baba, angepaswa kukabidhi usukani kwa mikono salama inayoweza kuendesha Mlima Kenya vyema, lakini hajafanya hilo.”

Kuhusu hatua ya Rais kuunga mkono muungano wa Nasa, Bi Wanjiru alisema Bw Kenyatta ana haki kidemokrasia kumuunga mkono kiongozi yeyote apendaye.

Kwa upande wake, alihoji kuwa kama mojawapo wa waasisi wa chama cha UDA, wamepania kupigia debe azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia ikulu mwaka ujao.

“Hiyo ni haki yake kisiasa kumuunga yeyote anayetaka. Lakini ni Wakenya wataamua nani atakuwa Rais, raia watawapigia kura viongozi wanaowataka. Ni haki yake kidemokrasia kuunga mkono, kufadhili na hata kusimama pamoja na kiongozi yeyote atakayechagua,”

“Kwa upande wetu, tunajua ni nani atakuwa mgombea wetu wa urais – Dkt William Ruto, ambaye tutajitahidi kwa vyovyote kuhakikisha anashinda uchaguzi,” alieleza Askofu huyo wa Jesus Is Alive Ministries (JIAM) huku akithibitisha kuwa atakuwa debeni kuwania ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya UDA mwaka ujao 2022.

Katika hatua inayoashiria hata zaidi hali ya kuyumbayumba Mlima Kenya, Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, aliwazomea vikali viongozi kutoka eneo hilo wanaopinga kutawazwa kwake kama msemaji wa eneo la Kati.

Aliwalenga hususan magavana Anne Waiguru (Kirinyaga) Mwangi Wa Iria (Murang’a), Mutahi Kahiga (Nyeri), Francis Kimemia (Nyandarua) na Waziri wa Kilimo Peter Munya, ambao wamepuuzilia mbali kutawazwa kwake na kundi la wazee wa jamii ya Agikuyu.

Akizungumza jana katika kanisa la St Peter’s Kaunjira National Independent Church of Africa (NICA) mjini Meru, Bw Muturi aliwashutumu viongozi hao kwa kukosea heshima wazee, utamaduni na haki ya kidemokrasia kulingana na Katiba.

Alisema kuwa atajitolea vilivyo kurejesha utulivu katika siasa za eneo la Kati kwa kuimarisha utangamano.

“Viongozi ni sharti wawe na nidhamu kuheshimu maoni ya wengine. Ni sharti uwe tayari kusikiza wengine baada ya kutoa kauli yako,” alisisitiza Spika Muturi.

Maelezo ya ziada na ALEX NJERU, DAVID MUCHUI

Habari zinazohusiana na hii