• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KRA kuuza mali ya KICC kulipia deni la Sh450m

KRA kuuza mali ya KICC kulipia deni la Sh450m

Na DAVID MWERE

HUENDA mali ya thamani ya mabilioni ya fedha ya Jumba la Kimataifa la Mikutano la Kenyatta (KICC) ikauzwa kulipia deni la Sh450.58 milioni linalodaiwa na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru (KRA), kwa kutolipa ushuru.

Hii ni licha ya kwamba KICC pia inadaiwa jumla ya Sh928.93 milioni na wafanyabiashara mbalimbali walioiuzia bidhaa kwa mkopo.

Kati ya fedha hizo, Sh928.93 milioni, karibu Sh686.32 milioni zinahusiana na bidhaa ambazo ziliwasilishwa kwa KICC wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa mataifa wanachama wa Shirika la Kibiashara Ulimwenguni (WTO) uliofanyika nchini kuanzia Desemba 15 hadi 19, 2015.

Ufichuzi kuhusu madeni ya KICC, likiwa shirika la kiserikali, unapatikana katika ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Nancy Gathungu kuhusu hali yake ya kifedha iliwasilishwa bungeni wiki jana.

Bi Gathungu katika ripoti hiyo anaonya kuwa kwa kufeli kulipa ushuru, KICC inaweza kutozwa faini na riba, mbali na kwamba itakuwa vigumu kwake kulipa deni hilo ikizingatiwa kuwa mapato yake yamepungua.

“Kufeli kulipa ushuru wakati ufaao kunaweza kuchangia KICC kutozwa faini kubwa na riba. Pia kuna uwezekano wa mali ya shirika hilo la serikali kuuzwa ili kulipia deni hilo,” akasema Bw Gathungu. Hii ni licha ya kwamba Bi Gathungu anashuku uhalali wa madeni hayo yanayoizonga KICC. Pesa ambazo KRA inadai KICC ni pamoja na ushuru wa zamani wa Sh22.9 milioni, ushuru uliojumuishwa wa Sh413.53 milioni na ushuru wa Sh14.1 milioni ambao ilipaswa kulipa katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019. Ripoti hiyo ya ukaguzi inasema kuwa thamani ya KICC ni Sh4.04 bilioni kwa mujibu wa ukadiriaji wa aina nne za mali yake katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

“Mkadiriaji thamani hakutoa ripoti yenye maelezo ya kina kuhusu jinsi shughuli hiyo ilivyoendeshwa. Hii ndio maana ardhi na majengo yalipewa thamani ya chini kuliko ile halisi,” Bi Gathungu akasema katika ripoti.

hiyo. Shughuli hiyo ya ukadiriaji thamani ya mali ya KICC iliyomgharimu mlipa kodi Sh7.6 milioni ilionyesha kuwa ardhi kulikojengwa KICC ni ya thamani ya Sh2.3 bilioni, majengo ni ya thamani ya Sh1.66 bilioni huku vifaa vya afisi vikigharimu jumla ya Sh76.5 milioni.

Thamani ya hiyo ya ardhi, hata hivyo, haikujumuisha ardhi ya eneo la uegeshaji kwa jina COMESA na eneo ambako kumewekwa mnara wa Rais wa kwanza nchini, Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

You can share this post!

Omar Hassan kupata ushindani mkali katika kuwania tiketi ya...

Ruto apigia debe mgombeaji wa UDA Kiambaa kupitia simu