• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
JAMVI: Raila kuvizia ziara za Rais Ukambani kwaibua hofu

JAMVI: Raila kuvizia ziara za Rais Ukambani kwaibua hofu

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ya kuandamana na Rais Uhuru Kenyatta alipozuru kaunti za Machakos na Makueni imewapa mchecheto washirika wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wanaohisi kwamba iliwaharibia fursa ya kushauriana na rais masuala ya kisiasa ya eneo lao.

Bw Musyoka alikiri mbele ya Rais Kenyatta kwamba hakutarajia kumuona Bw Odinga kwenye ziara hiyo huku wadadisi wakisema kiongozi wa nchi alitaka kutoa ujumbe kwa viongozi wa kisiasa wa Ukambani kwamba anampendelea waziri mkuu huyo wa zamani kuwa mrithi wake.

Bw Odinga na Bw Musyoka wamekuwa wakitofautiana kuhusu mkataba wa muungano wa NASA wa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017. Kiongozi wa Wiper anasema kwamba Bw Odinga alimsaliti kwa kukataa kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kwa upande wake, Bw Odinga anadai kwamba hitaji hilo katika mkataba wa NASA lilipitwa na wakati kwa kuwa hawakuunda serikali.

Bw Musyoka anaunga mkono handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta lakini ameapa kuwa hatamuunga mkono kiongozi huyo wa ODM kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa mara ya tatu.

Vyama vyao vinashirikiana na Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta na ODM imeanza kusuka muungano na chama hicho tawala huku Wiper kikishirikiana na Kanu, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya kubuni muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Kulingana na washirika wa Bw Musyoka, kujitokeza kwa Bw Odinga kwenye ziara ya Rais Ukambani kulimharibia kiongozi wao aliyetaka kutumia ziara hiyo kupigia debe azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022 kwa kuonekana kuungwa mkono na rais.

Seneta wa Kitui Enock Wambua ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka alisema kwamba Bw Odinga aliwadharau kwa kuzuru eneo hilo bila kualikwa.

“Tulishangaa kumuona Bw Odinga katika mkutano (katika eneo kunakojengwa bwawa la Thwake) ilhali tulitaka kuzungumza kivyetu na rais kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi ya eneo letu,” Bw Wambua alisema na kuongeza kuwa kujitokeza kwa Bw Odinga kuliwaharibia mipango yao.

Mchanganuzi wa siasa, Geff Kamwanah anasema kauli za wanasiasa wa Wiper ni sehemu ya siasa za kumrithi Rais Kenyatta kati ya Bw Odinga na Bw Musyoka.

“Wawili hao wanawania baraka za Rais Kenyatta na kwa hivyo, kujitokeza kwa Bw Odinga eneo la Ukambani kwa mwaliko wa rais, hakukufurahisha Bw Musyoka na washirika wake,” asema Bw Kamwanah.

Mchanganuzi huyu anasema kwamba hasira za washirika wa Bw Musyoka kwa Bw Odinga zinatokana na ujumbe ambao Rais Kenyatta alitaka kuwasilisha kwa kumwalika mshirika wake wa handisheki kwenye ziara yake Ukambani.

Kumekuwa na minong’ono kwamba Rais Kenyatta anawashawishi vinara wa OKA, akiwemo Bw Musyoka na vinara wenza katika NASA, kuungana chini ya Bw Odinga ili waweze kumshinda Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa Bw Odinga anasema kwamba hajatangaza azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, ameashirika nia yake ya kuendelea kushirikiana na Bw Musyoka.

Mbunge wa Mwingi North Musembi Nzengu, anasema kwamba Bw Odinga anafaa kuzungumza moja kwa moja na Bw Musyoka iwapo anataka kuungwa mkono na wakazi wa eneo la Ukambani.

Bw Kamwanah anasema kinachowauma wandani wa Bw Musyoka ni kuwa Rais Kenyatta hakualika vigogo wengine wa upinzani kwenye ziara yake eneo la Nyanza alikoanzisha miradi mikubwa ya maendeleo.

“Uwepo wa Bw Odinga ulivuruga mipango ya Bw Musyoka na hii ndiyo imefanya washirika wake kueleza kiongozi wao alivyohisi. Lakini ninasisitiza kuwa nia ya rais ilikuwa ya kuwasilisha ujumbe kwa viongozi wa Ukambani kwamba anamtambua Bw Odinga zaidi ya anavyomtambua Bw Musyoka,” asema na kuongeza: “Wanafaa kumlaumu rais kwa kumwalika Bw Odinga kwa kuwa hiyo ilikuwa ziara ya rais.”

Kulingana na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua ambaye ni hasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka eneo la Ukambani na ambaye pia ametangaza azima ya kugombea urais, Bw Odinga ni kiongozi wa kitaifa na wanaomlaumu kwa kujitokeza kwenye ziara ya rais eneo la Ukambani wanajidunisha.

“Bw Odinga ana haki ya kutembelea eneo lolote bila ruhusa kwa sababu ni kiongozi wa kitaifa,” asema.

Duru zinasema ingawa Rais Kenyatta anataka vigogo wa kisiasa wanaomuunga kuunda muungano mkubwa wa vyama vya kisiasa kumkabili Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, washirika wa Bw Musyoka wamekuwa wakimshinikiza asikubali kwa urahisi kuungana na Bw Odinga.

“Kuna kitu ambacho Bw Musyoka anaficha washirika wake kwa sababu amekuwa akizungumza na Bw Odinga bila kuwahusisha. Hii ndiyo sababu alikuwa mwepesi wa kusema mbele ya rais kwamba hajaketi na Bw Odinga kuzungumzia uchaguzi wa 2022,” asema mbunge mmoja wa Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Alisema kwamba Rais Kenyatta anatumia mbinu aliyotumia kwenye mazungumzo yaliyozaa handisheki yake na Bw Odinga kuwaleta pamoja vigogo wa kisiasa hasa vinara wenza wa NASA ambao wameshinikizwa na washirika wao kuchukua misimamo mikali kuhusu 2022.

Rais Kenyatta na Bw Odinga hawakuhusisha washirika wao wa kisiasa waliokuwa na misimamo mikali kwenye mazungumzo yaliyozaa handisheki yao ya Machi 2018.

You can share this post!

Vieira aanza kazi kambini mwa Palace kwa ushindi dhidi ya...

DINI: Ugumu wa maisha usikufanye upoteze imani au kulaumu...