• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Corona: Uhaba wa vifaa vya upimaji nchini

Corona: Uhaba wa vifaa vya upimaji nchini

HELLEN SHIKANDA na ANGELA OKETCH

SERIKALI imepunguza idadi ya watu wanaopimwa virusi vya corona kwa siku kutokana na ukosefu wa vifaa vya kupimia.

Idadi ya watu wanaopimwa virusi vya corona imepungua kutoka 8,000 hadi 5,000 kwa siku.Jumla ya watu milioni 2 wamepimwa virusi vya corona tangu kisa cha kwanza kuripotiwa nchini mnamo Machi 23 mwaka jana.

Kutokana na idadi ndogo ya watu wanaopimwa virusi hivyo, vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, kuna hatari ya uenezaji zaidi wa maambukizi nchini.Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (Kemri) ina uwezo wa kupima sampuli 35,000 kwa siku.

Lakini kwa miezi miwili sasa imekuwa ikipima chini ya watu 100 kwani haijapokea vifaa vya kuendesha shughuli hiyo kutoka kwa serikali.“Kwa miezi miwili sasa, sitaki kukudanganya, hatujakuwa tukipima virusi vya corona.

Tunapima tu watu wanaotaka kusafiri, husasan, watafiti wetu. Hatuna vifaa vya kupimia virusi vya corona,” akasema afisa wa Kemri aliyeomba jina lake libanwe kwa kuhofia kuandamwa na serikali.

Afisa huyo alihoji kwamba taasisi ya Kemri imesalia na vifaa 300 pekee vya kupima corona.“Mashine za kupima corona hazina kazi kwani hatuna kemikali na viungo vingine hitajika.

Tunasubiri serikali ituletee vifaa ili tuanze tena kupima wananchi,” akasema.Serikali pia iliacha mpango wake wa kutafuta watu waliotangamana na waathiriwa wanaopatikana na virusi vya corona.

Hata hivyo, Lakini Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Francis Kuria, alieleza kuwa sera ya serikali inasema ni watu tu wanaoonyesha dalili za virusi vya corona ndio wanahitaji kupimwa.Kenya imekumbwa na uhaba wa vifaa vya kupima corona huku nchi ikiwa katika hatari ya kupatwa na wimbi la nne la janga hilo.

Dkt Kuria aliongeza kuwa Mamlaka ya Kusambaza Vifaa vya Matibabu Nchini (Kemsa) ilipokea vifaa 650,000 vya kupima corona Jumatatu, ambavyo vilipelekwa katika maeneo mbalimbali ya nchi siku ya Jumatano.

Alikanusha ripoti kwamba baadhi ya vifaa vimekwama bandarini.“Vifaa vya kupima corona vilitua nchini kwa ndege. Kama kuna vilivyokwama bandarini mimi sijasikia,” akasisitiza.Dkt Ahmed Kalebi, mtaalamu wa matibabu ya virusi, asema hatua ya kupima idadi ndogo ya watu huenda ikazua hatari siku za usoni.

“Inamaanisha kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaotembea na virusi vya corona bila kujua, na kuisambaza zaidi,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Ajowi, Akinyi wafuzu kwa raundi 2 bila jasho Tokyo

Mahakama iko msalabani sasa,alalama Koome