• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
WASONGA: Masomo yasivurugwe tena mwaka huu mfupi

WASONGA: Masomo yasivurugwe tena mwaka huu mfupi

Na CHARLES WASONGA

MWAKA wa masomo wa 2021 unaaanza leo shule zote zinapofunguliwa kwa muhula wa kwanza kwa madarasa yote katika shule za msingi na upili.

Hii ni kulingana na mwongozo wa uliotolewa na Wizara ya Elimu kabla ya shule kufungwa Julai 16 kwa likizo fupi ya siku 10 baada ya kukamilishwa kwa mwaka wa masomo wa 2020.

Mwaka huo uliathirika na janga la Covid-19 lililochangia kukatizwa kwa shughuli za masomo kwa miezi saba tangu Machi 15, 2020 hadi Oktoba 5, 2020.

Ni kutokana na changamoto hii ambapo Wizara ya Elimu imepunguza muda wa masomo katika mwaka wa masomo unaoanza leo, kutoka wiki 39 hadi wiki 30.

Ndiposa kulingana na mwongo huo mpya, wanafunzi wanaojiunga na darasa la nane kuanzia leo watafanya mtihani wao wa kitaifa (KCPE) kuanzia Machi 22 hadi Machi 24, mwaka ujao. Kwa upande mwingine wenzao wa kidato cha nne watafanya mtihani wao (KCSE).

Ni kwa msingi huu ambapo nawashauri wanafunzi, wazazi, walimu, bodi simamizi za shule, serikali na wadau wengine katika sekta ya elimu kuhakikisha kuwa utulivu unadumishwa shuleni katika kipindi hiki.

Visa vya masomo ya wanafunzi kukatizwa kwa misingi ya sababu mbalimbali, kama vile, kutokea kwa ghasia za wanafunzi, kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi wasiokamilisha kulipa karo miongoni mwa sababu nyinginezo vidhibitiwe.

Changamoto kama hizi zishughulikiwe mapema ili zisiathiri masomo na malengo ya walimu na wanafunzi kukamilisha silabasi ya mwaka huu wa masomo.

Naamini kuwa fujo za wanafunzi, ambazo aghalabu husababisha uharibifu wa mali shuleni, zinaweza kudhibitiwa mapema kabla ya kutokea ikiwa walimu wakuu na walimu watadumisha mashauriano ya kila mara kati yao na wanafunzi.

Kwa mfano, kupitia viranja, walimu wakuu wanaweza kupata habari kuhusu yale yanayowakera wanafunzi ili kuchukua hatua za haraka kabla ya wao kuamua kuzuia fujo ili wasikizwe.

Vile vile, walimu na wafanyakazi wengine wa shule, haswa zile za mabweni, wanafaa kuwa macho ili kuwatambua mapema wanafunzi watovu wa nidhamu na waraibu wa pombe na dawa za kulevya.

Kulingana na ripoti ya jopo kazi lilichunguza kiini cha visa vya fujo shuleni na uteketezaji wa mabweni mnamo 2016, mapuuza ya walimu wakuu yalitajwa kama mojawapo ya sababu zilichangia kutokea kwa visa hivyo. Katika mwaka huo, kuliripotiwa zaidi ya visa 107 vya wanafunzi kuteketeza mabweni na majengo mengine ya shule wakilalamikia masuala mbalimbali.

Jopokazi hilo, lililoongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mashariki Bi Claire Omollo, ilipendekeza kuwa walimu wakuu wa shule za upili wamakinike zaidi na waishi ndani au karibu na shule zao ili kung’amua haraka malalamishi ya wanafunzi wao.

Vile vile, shule za upili, haswa zile za mabweni, zilishauriwa kubuni idara mahsusi za kutoa ushaurinasaha kwa wanafunzi waliogunduliwa kupotoka kimaadili kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya pombe na mihadarati.

Visa kama hivi havifai kushuhudiwa katika shule za humu nchini katika mwaka kama huu wa masomo ambao ni mfupi ili wanafunzi na walimu wapate muda tosha wa kukamilisha silabasi.

Kwa upande mwingine, walimu wakuu wakome kuwatuma nyumbani wanafunzi, haswa wale wa kidato cha nne na darasa la nane, kwa kutokamilisha kulipa karo. Wabuni njia mbadala za kuwashurutisha wazazi kulipa karo, badala ya kukatiza masomo ya wanafunzi.

You can share this post!

WARUI: Walimu wakuu wanaokaidi agizo la karo wachukuliwe...

TAHARIRI: Bunge liharakishe sheria ya umasikini