• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
WARUI: Walimu wakuu wanaokaidi agizo la karo wachukuliwe hatua

WARUI: Walimu wakuu wanaokaidi agizo la karo wachukuliwe hatua

Na WANTO WARUI

INASHANGAZA kusikia baadhi ya walimu wakuu wa sekondari wanakiuka mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu kuhusu karo ya shule.

Katika mwongozo huo ambao umepunguza karo kwa kiwango kidogo, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alieleza sababu za kufanya hivyo.

Hizo ni pamoja na kuwapunguzia wazazi mzigo wakati huu wa hali ngumu ya kiuchumi iliyotokana na janga sugu la Covid-19.

Aidha Waziri alitoa onyo kwa walimu wakuu wasiongezee karo ya shule.

Licha ya hayo, kuna baadhi ya walimu wakuu wa shule za upili ambao wameenda kinyume na maagizo hayo na kutoza wazazi ada ya ziada. Kuna tetesi kuwa shule ya Wasichana ya Tumutumu, Nyeri, ni mojawapo ya shule zinazodai malipo hayo.

Walimu wanadai kuwa kuna malipo mengine yanayohitajika shuleni kama vile ya michezo au ya kulipia walimu walioajiriwa na Bodi za Shule.

Sababu yoyote ile inayotolewa na walimu hawa haina mashiko kamwe na huku ni kukosa utu kabisa na kuwa na tamaa ya pesa.

Kwa sasa, muda wa masomo katika kila muhula umepunguzwa sana kwa kiasi cha zaidi ya mwezi mzima.

Kwa mfano, Waziri wa Elimu alisema kuwa muhula ujao wa kwanza unaoanza leo utakuwa na majuma 30 badala ya 39.

Hivi ni kusema kuwa muhula huo umepunguzwa kwa mwezi mzima na wiki moja.

Inakuwaje mwalimu mwenye maadili akaongezea karo?

Vilevile, mwaka mmoja wa masomo sasa una mihula minne kinyume na hapo awali ambapo mwaka mmoja ulikuwa na mihula mitatu.

Zaidi ya hayo, wazazi hawapati muda wa kujitayarisha na kutafuta karo kama ilivyokuwa hapo awali.

Shule zilifungwa kwa wiki moja tu na ni katika wiki hiyo ambapo mzazi anatarajiwa alipe karo ya muhula wa kwanza ujao, anunue vitabu vipya vya kusomea na mahitaji mengine muhimu ya masomo.

Je, ni kusema kuwa walimu hawa hawaoni hivi?

Kwa muda mrefu, baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakifanya ufisadi kama huu shuleni mwao na wakati ni sasa ambapo tabia hizi mbaya zinastahili kukomeshwa.

Shule zinahitaji kuandaa bajeti zao mapema na kuzikabidhi kwa Wizara ya Elimu ili wizara ielewe na ishughulikie mahitaji hayo ya shule.

Hata katika shule nyingi utakuta kuwa ada za ziada zinazotozwa wazazi si za maendeleo yoyote ya shule kamwe bali ni mbinu haramu za walimu wakuu za kujitafutia marupurupu.

Vitendo kama hivi vnafaa kulaaniwa na viongozi wote nao walimu kama hawa ambao hawana utu wala uchungu wa mzazi wachukuliwe hatua za kisheria.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Mahangaiko tele ya kupata tiba yalazimu...

WASONGA: Masomo yasivurugwe tena mwaka huu mfupi