• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wito wagonjwa wa kawaida wazuru hospitali nyinginezo idadi ya wagonjwa wa Covid-19 ikiongezeka katika hospitali ya Tigoni

Wito wagonjwa wa kawaida wazuru hospitali nyinginezo idadi ya wagonjwa wa Covid-19 ikiongezeka katika hospitali ya Tigoni

Na LAWRENCE ONGARO

IDADI ya wagonjwa wa Covid-19 inazidi kuongezeka katika hospitali ya Tigoni, Kaunti ya Kiambu.

Kwa wiki mbili zilizopita, wagonjwa wapatao 19 wamelazwa katika hospitali hiyo kutokana na Covid-19.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro amesema tayari wametoa amri wagonjwa wa kawaida wazuru hospitali nyinginezo ili wasijumuike na walioambukizwa Covid-19.

“Kwa hivyo, hospitali hiyo itawahudumia wagonjwa wa Covid-19 pekee kwa wakati huu. Tunataka wagonjwa wa kawaida wasikaribiane na wale wa corona,” alisema Dkt Nyoro.

Kulingana na madaktari katika hospitali hiyo, wagonjwa wengi ni wale walio na umri wa juu, hali inayostahili kudhibitiwa haraka.

Alisema hadi wakati huu, wagonjwa wapatao 150 wamelazwa katika hospitali ya Tigoni wakiugua Covid-19.

Dkt Nyoro alisema mwezi mmoja uliopita, kulikuwa na wagonjwa tisa pekee walioambukizwa Covid-19, lakini wiki chache zilizopita, mambo yamebadilika kabisa.

“Kulingana na hali ilivyo, afisi ya kaunti itafanya mkutano wa dharura na maafisa wa afya ili kujadiliana kuhusu hali ya Covid-19 na jinsi ya kuitatua,” alisema Dkt Nyoro.

Alitoa wito kwa wananchi popote pale walipo wafuate maagizo yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya.

Alitahadharisha wananchi wasichukulie jambo hilo kwa mzaha kwa sababu Covid-19 inasambaa kwa kasi.

Alithibitisha kuwa hospitali ya Tigoni ina vitanda 330 vya wagonjwa wanaougua homa ya Covid-19.

Waziri wa afya wa kaunti hiyo Dkt Joseph Murega alisema kaunti hiyo iko imara kuona ya kwamba inatibu wagonjwa wote wanaougua Covid-19.

“Madaktari watafanya juhudi kuona ya kwamba wanawatibu wagonjwa hao hadi wapate nafuu. Wauguzi pia wako mstari wa mbele kuona shughuli hiyo inafanikiwa jinsi ipasavyo,” alisema Dkt Murega.

  • Tags

You can share this post!

Wafugaji na wafanyabiashara wahimizwa kutathmini namna ya...

Bermuda yawa nchi ya kwanza ndogo zaidi kuwahi kuzoa medali...