• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
BBI: Uhuru, Raila sasa kusuka mbinu mpya ya mageuzi

BBI: Uhuru, Raila sasa kusuka mbinu mpya ya mageuzi

Na WANDERI KAMAU

KUHARAMISHWA kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) na Mahakama ya Rufaa kunatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kwa siasa za Kenya, uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Wale walioathiriwa sana na uamuzi huo ni Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM, Raila Odinga na muungano wa Okoa Kenya Alliance (OKA).

Kulingana na wadadisi wa siasa, huenda Rais Kenyatta na Bw Odinga wakabuni mbinu mpya za kuendeleza mageuzi ya kikatiba waliyotaka kupitia Bunge la Kitaifa.

Wanasheria na wataalamu wa Katiba wamekuwa wakisisitiza kuwa si kila mapendekezo yaliyojumuishwa kwenye mpango huo ambayo yalihitaji kupitishwa kupitia refarenda.

“Kuna uwezekano Rais Kenyatta na Bw Odinga kupitisha vipengele ambavyo havihitaji kupigiwa kura na wananchi. Kupitia mbinu hii, watawashinikiza wabunge wao kuungana ili kupitisha mapendekezo hayo. Hivyo, huenda huo usiwe mwisho wao kusukuma matakwa yao,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mdadisi wa sheria.

Hatua nyingine ambayo Rais Kenyatta anatarajiwa kuchukua ni kufanya mageuzi katika baraza la mawaziri, ili kubuni serikali ambayo inaonekana kuashiria taswira ya kitaifa.

Wadadisi wanasema hatua hiyo itakuwa kama njia ya kuwajumuisha vigogo wa muungano wa OKA na washirika wao kwenye serikali yake, ili wasishawishike kujiunga na Naibu Rais William Ruto.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).Kwa majuma kadhaa, kumekuwa na uvumi kwamba huenda Rais Kenyatta akatekeleza mageuzi hayo.

Duru zimekuwa zikieleza lengo kuu la mabadiliko hayo ni kuwafurusha mawaziri, manaibu wa mawaziri na makatibu wa wizara ambao wanadaiwa kuegemea ama kuwa washirika wa Dkt Ruto.

“Bila shaka, uamuzi wa BBI ni pigo kubwa kwa karata za urithi za Rais Kenyatta, kwani alikuwa akitegemea maamuzi yatakayotolewa kubuni muungano wa kisiasa ambao ungemsaidia kumwachia uongozi Bw Odinga. Vinara wa OKA pia walitarajia kufaidika pakubwa kwa nyadhifa ambazo zingebuniwa,” asema Dkt Sang.

Hivyo, anasema huenda tukashuhudia miungano mipya ya kisiasa, hata miongoni mwa wanasiasa ambao hawangedhaniwa kuungana.

You can share this post!

BBI: Ruto asifu mahakama na kumshauri Uhuru

Lusaka apuuza uvumi anamezea useneta Bungoma