• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
GWIJI WA WIKI: Fred Mutwiri

GWIJI WA WIKI: Fred Mutwiri

Na CHRIS ADUNGO

MSHUMAA hauzimiki kwa kuuwasha mwingine.

Maisha ni safari na safari ni hatua. Safari ya kitalifa kirefu huanza kwa hatua moja.

Kabla ya binadamu kupiga hatua yoyote safarini, huwa tayari ameipiga hatua hiyo akilini mwake. Kwa hivyo, ni dhahiri shahiri kuwa mtu afikirivyo ndivyo alivyo. Uko jinsi ulivyo leo kwa sababu wewe mwenyewe uliamini utakuwa hivyo tangu jana. Vyovyote vile uwavyo, jinsi utakavyokuwa kesho ni matokeo ya jinsi unavyoamini leo kuhusu hiyo kesho yako.

Jihisi kuwa mwenye thamani kwa sababu umeibeba sura ya Mungu aliyekuumba kwa mfano wake mwenyewe. Usikubali kushindwa na lolote maishani.

Katika kila ufanyacho au unachotarajia kutenda, ukitanguliza mawazo ya kushindwa, haitakuwa rahisi kufaulu.

Kama ambavyo neno litokalo kwa Mungu linavyoweza kuumba, ndivyo maneno ya kutoka vinywani mwetu pia yanavyoweza kutujenga au kutubomoa.

Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi. Kila tunachokiri ndicho hutokea. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mawazo ya mtu na maneno ayanenayo. Ayazungumzayo mtu ndio yanayoujaza moyo wake.

Tofauti kati ya kuku na tai ni nia. Penye nia pana njia. Ni wajibu wa kila mja kuteua iwapo anataka kuwa kuku asiyepaa ama tai anayepaa upeo wa kupaa. Kufaulu kwako ni zao la juhudi. Bahati ni chudi na nidhamu ndiyo dira kamili katika maisha.

Azimia kutimiza ndoto zako kwa kuwa mafanikio hayaji kwa kulaza damu bali kwa kupinda mgongo na kujifunga kibwebwe.

Huu ndio ushauri wa Bw Fred Mutwiri – mwanafunzi wa shahada ya uzamifu na mwandishi mahiri anayefundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls, Kaunti ya Makueni.

MAISHA YA AWALI

Mutwiri alizaliwa mnamo 1992 katika kitongoji cha Nkandone, Kaunti ya Meru. Ndiye mtoto wa sita katika familia ya Bi Martha Kabiro na Bw John Ngore.

Hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani ya Mutwiri tangu utotoni. Alikuwa mwepesi wa kusoma habari shuleni na kanisani huku akiiga sauti za watangazaji maarufu wa redioni. Alistahiwa pakubwa na wanafunzi na waumini kwa upekee wa kipaji chake cha ulumbi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nkandone, Meru. Alisomea huko hadi darasa la saba kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Naathu, Meru. Nusura ndoto zake za masomo ziyeyushwe na pigo la kufariki kwa baba mzazi mnamo 2004.

Kwa imani kwamba penye mawimbi na milango ya heri i papo hapo, Mutwiri alianza kuishi kwa kumtegemea mama mzazi ambaye hakuwa na kazi yoyote ya staha na haiba.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) katika Shule ya Upili ya Igembe Boys, Meru mnamo 2009 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anakiri kuwa mapenzi yake kwa masomo ya lugha ni zao la kuhimizwa mara kwa mara na Bw Irai aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili. Wengine waliochangia ari yake ya kukichapukia Kiswahili ni Prof Rayya Timammy, Dkt Ongarora na marehemu Prof Ken Walibora.

UALIMU

Mutwiri alianza kufundisha mnamo 2013 akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Chuka kuanzia 2015. Alifuzu mwaka wa 2019 baada ya kuwasilisha tasnifu “Muundo wa Sentensi ya Kiigembe: Mtazamo wa Eksibaa” chini ya usimamizi wa Prof John Kobia na Dkt Allan Mugambi.

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo 2017 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya St Lawrence Nziu Girls Makueni. Baada ya kukamilisha shahada ya uzamili, Mutwiri alirejea katika Chuo Kikuu cha Chuka mnamo 2020 kwa minajili ya shahada ya uzamifu (phD). Analenga kufuzu mnamo 2022.

UANDISHI

Mutwiri alikuwa na mazoea ya kuandika hadithi za kubuni pamoja na mashairi alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Utashi wake wa kuandika ulichochewa zaidi na wahadhiri wake wa shahada ya uzamili wakiwemo Prof Kobia, Dkt Erastus Miricho na Bw Bitugi Matundura.

Waliomhimiza aanze kuchapisha kazi zake ni marehemu Bernard Omwega Osano (Kaka Benosa) aliyekuwa mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Moi Girls Nairobi na Bw Timothy Omusikoyo Sumba – mwandishi stadi na mhariri mzoefu wa vitabu vya Kiswahili.

Kufikia sasa, Mutwiri amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida ya kitaifa na kimataifa.

Mwalimu Fred Mutwiri. Picha/ Chris Adungo

Alishirikiana na Prof Miriam Mwita wa Chuo Kikuu cha Mashariki ya Afrika Baraton kuandika makala ‘Usawiri wa Wahusika wa Jinsia ya Kiume katika riwaya ya Chozi la Heri’ na yakafyatuliwa katika jarida Mwanga wa Lugha’.

‘Muundo wa Virai vya Sentensi ya Kiigembe’ ni makala aliyoandika kwa kushirikiana na Dkt Allan Mugambi na yakachapishwa na ‘East African Scholars Journal of Education, Humanities and Literature’.

Mbali na riwaya ‘Joka Kitandani’, Mutwiri ameandika kitabu ‘Fumbo la Fasihi’ na msururu wa vitabu vya mazoezi na marudio ‘Futari Njema ya Fasihi Simulizi’, ‘Futari Njema ya Isimujamii’, ‘Futari Njema ya Kigogo’, ‘Futari Njema ya Chozi la Heri’ na ‘Futari Njema ya Tumbo Lisiloshiba’.

Aidha, ametunga hadithi fupi ‘Sumu Tamu’, ‘Karakana ya Upatanisho’, ‘Ningali Hai’, ‘Fumbo la Fumba’, ‘Bibi wa Tajiri’, ‘Si Ndoto Tena’, ‘Joka la Baharini’ na ‘Nzige’.

‘Siri ya Insha’ ni kitabu ambacho Mutwiri aliandika kwa pamoja na Bw Steven Mativo na mwalimu Allan Babashi wa Starehe Boys Centre & School mnamo 2021.

Baadhi ya mashairi yake yamechapishwa katika diwani ‘Malenga wa Afrika’ iliyohaririwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Timothy Omusikoyo Sumba na Fatma Ali Mohammed kutoka Zanzibar.

Mutwiri anatarajia kutoa kitabu ‘Fumbo la Sarufi Mtindo wa KCSE’ mwaka huu 2021.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Mutwiri ni kuweka hai ndoto yake ya kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri katika vyuo vikuu.

Anajivunia kuelekeza idadi kubwa ya chipukizi katika sanaa ya uandishi kupitia ‘YouTube’ (Mutwiri Fred).

Kwa pamoja na mkewe, Bi Ruth Kaimuri, wamejaliwa mtoto mmoja: Mellisa Gatwiri.

You can share this post!

Polisi wanne wanaoshtakiwa kwa mauaji wapatwa na Corona...

Real Madrid waponda Mallorca na kurejea kileleni mwa...