• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Afueni ya muda kwa wasafiri katika kaunti zilizowekwa ‘lockdown’

Afueni ya muda kwa wasafiri katika kaunti zilizowekwa ‘lockdown’

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imetoa agizo jipya kuhusu marufuku ya kuingia na kuondoka kaunti za Nairobi, Nakuru, Kajiado, Machakos na Kiambu iliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta, Ijumaa.

Jumamosi msemaji wa serikali Cyrus Oguna ametangaza kuwa wale ambao wanataka kuondoka au kuingia kaunti hizi tano sasa wamepewa muda zaidi wa hadi Jumapili, Machi 28, 2021, kufanya hivyo.

“Wale ambao marufuku haya yalianza kutekelezwa ikiwa hawajajiandaa wamepewa muda wa hadi kesho (Jumapili) saa mbili usiku wasafiri. Wale wanaotaka kuingia na kuondoka kaunti hizo tano wamepewa muda wa hadi siku na wakati huo kusafiri,” Bw Oguna akawaambia wanahabari katika jumba la Teleposta, Nairobi, Jumamosi.

Mnamo Ijumaa Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa marufuku hiyo ambayo inalenga kuzuia msambao wa virusi vya corona ingeanza kutekelezwa usiku wa manane.

Baada ya tangazo hilo watu waliokuwa wakitaka kusafiri kutoka na kuingia Nairobi waliingiwa na wasiwasi na wakaanza kutafuta magari ya usafiri ambayo pia yalitoza nauli ya juu zaidi.

Kwa mfano, wale ambao walikuwa wakisafiri kutoka Nakuru kuja Nairobi walikuwa wakitozwa nauli ya kati ya Sh2,500 na Sh3,000 badala ya nauli ya kawaida ya Sh600.

Na wale ambao walikuwa wakisafiri kwenda Kisumu walikuwa wakitozwa nauli ya Sh5,000 badala ya Sh1,500.

Hii ni licha ya kwamba Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya Rais Nzioka Waita kufafanua kuwa kaunti hizo tano zinachukuliwa kama eneo moja na sio marufuku kwa watu kusafiri kati yazo.

Kwa mfano, watu wako huru kusafiri kutoka Nairobi kwenda Nakuru au kutoka Kiambu kwenda Kajiado. Lakini watu kutoka kaunti hizo tano hawaweza kuruhusiwa kwenda kaunti zingine 42 kwa barabara, reli au kwa ndege.

Bw Oguna Jumamosi alisema kuwa vizuizi vya polisi vitawekwa katika mipaka ya kaunti hizo tano (Nairobi, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nakuru) ili kuzuia watu kuingia na kuondoka maeneo hao.

You can share this post!

UoN yafungwa

Atletico, Sevilla na Roma katika vita vya kuwania saini ya...