• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Aliyeuawa kinyama alituzwa na Rais 2016

Aliyeuawa kinyama alituzwa na Rais 2016

Na WAANDISHI WETU

MFUGAJI hodari wa Pwani ambaye alikuwa mmoja wa watu watatu waliouawa kinyama eneo la Junju, Kaunti ya Kilifi wiki iliyopita, alikuwa ametuzwa na Rais Uhuru Kenyatta kwa uhodari wake wa ufugaji.

Jana, diwani wa zamani, Bw Onesmus Gambo alikuwa miongoni mwa washukiwa waliofikishwa kortini kwa madai ya kuhusika kwa mauaji hayo.

Alifikishwa mahakamani Shanzu pamoja na Bw Raphael Kenneth Lewa ambaye polisi wanadai ni mmoja wa maskwota wanaoishi katika ardhi ambayo watatu hao walikuwa wameenda kutazama.

Jana, Mahakama iliagiza Bw Gambo awekwe kizuizini kwa siku 14 uchunguzi ukiendelea.

Diwani huyo wa zamani alijitetea kwamba ijapokuwa aliwahi kufanya mikutano na wanakijiji, hakuhusika kupanga mauaji.

Katika kisa cha Jumatano iliyopita kilichotokea Wadi ya Junju, eneobunge la Kilifi Kusini, wanakijiji walishambulia na kuua mfanyabiashara huyo mashuhuri Sidik Anwarali Sumra, dereva wake Rahil Mohammed Kasmani na Bw James Kazungu kafani aliyekuwa wakala wa ardhi.

Bw Sumra, 48, aligonga vichwa vya habari Pwani wakati alipotuzwa na Rais Kenyatta katika maonyesho ya kilimo Mombasa mwaka wa 2016, kwa kuibuka mfugaji bora zaidi wa ng’ombe.

Awali Jumatatu, washukiwa 13 walifikishwa mahakamani akiwemo mzee wa kijiji Philip Ziro Lewa.

Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani, polisi walisema wanamchukulia Bw Gambo kama mshukiwa kwa vile wanaamini alikutana na wafanyabiashara hao mwezi uliopita wakajadiliana kuhusu nia yao ya kununua ardhi eneo hilo.

Ripoti za polisi zimeonyesha kuwa baada ya kuuliwa, miili yao ilifungwa kwa pikipiki ambayo iliwaburuta hadi barabarani. Baadhi ya wanakijiji walitaka kuwachoma lakini wengine wakapinga.

Imebainika kuwa, gari lao liliporwa kabla kuchomwa, huku washukiwa pia wakiiba bunduki ya Bw Sumra.

Viongozi wa Kaunti ya Kilifi wamezidi kulaani mauaji hayo huku wakiyahusisha na uchochezi kuhusu mizozo ya ardhi.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi alisisitiza kuwa kila mwananchi ana haki ya kuishi katika kaunti hiyo bila kujali kabila lake na kuna njia za kisheria kutatua mizozo ya ardhi bila kushambulia watu.

“Hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kwenda Junju na wenyeji wanamjua. Alikuwa ameenda kutazama kipande cha ardhi kwa sababu alitaka kupanua biashara yake ya ufugaji. Huu ni ukatili ambao haufai kushuhudiwa katika enzi hizi,” akasema.

Familia ya Bw Kafani sasa inadai haki na waliohusika katika mauaji hayo waadhibiwe.

Ripoti za Brian Ocharo, Maureen Ongala, Wachira Mwangi na Alex Kalama

  • Tags

You can share this post!

Kiambaa kuamua mwelekeo wa Nyoro kisiasa – Wadadisi

Nani atapaa Kiambaa?