• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Asilimia 40 ya wanawake Maragua, Murang’a ni walevi, serikali yafichuka

Asilimia 40 ya wanawake Maragua, Murang’a ni walevi, serikali yafichuka

NA MWANGI MUIRURI 

ASILIMIA 40 ya wanawake mjini Maragua ni walevi kupindukia wakitajwa hukesha kwenye mabaa, kamati ya Kiusalama Murang’a Kusini imesema.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini, Bw Gitonga Murungi alisema takwimu hizo zimetokana na idadi ya washukiwa wa ulevi ambao wamekamatwa katika kipindi cha wiki mbili sasa.

“Tumekuwa tukiendeleza msako wa kiusalama katika mji huu ambao katika siku za hivi karibuni umekuwa na changamoto za kiusalama. Katika misako hiyo, tubaini asilimia 40 ya tunaokamata ni wanawake,” akasema.

Bw Murungi alisema hali hiyo inazua wasiwasi mkuu kuhusu uwezo wa Mji wa Maragua kuwa na wake na walezi wa watoto ikiwa asilimia ya juu hivyo ya wanawake imezama ndani ya ulevi.

“Usiku wa kuamkia Septemba 3, 2023 tumetekeleza msako katika baa za Maragua, kati ya washukiwa 15 ambao tumenasa, sita ni wanawake. Hata kuna visa ambapo wanawake huwa ndio wengi katika orodha ya waliokamatwa,” akasema.

Alisema kwamba misako hiyo ya kuvunja mitandao ya kuzurura mjini kwa nia zisizoeleweka, ulevi, mihadarati na ukahaba itaendelea kutekelezwa.

Aidha, alisema kwamba baa zote ambazo zimehusishwa na ukiukaji wa sheria na hata baada ya kupewa onyo zinakaidi, zitafungwa.

“Tayari tumelifunga baa la Coro baada ya kutuhumiwa kuwa kiini cha ujambazi wa mauaji, wizi wa kimabavu na pia kuchochea maovu ya ukahaba na mihadarati. Kwa sasa tumeagiza mwenye baa hiyo akome biashara hiyo huku tukitathmini hali,” akasema.

Bw Murungi alisema kwamba wote ambao hukamatwa katika misako hiyo ni lazima wafike mahakamani.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Kongamano: Serikali yaimarisha usalama

Serikali kupeleka wakulima kadha Colombia kujifunza...

T L