• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Askofu awaita walevi kanisani wapate mafundisho ya kidini

Askofu awaita walevi kanisani wapate mafundisho ya kidini

NA LAWRENCE ONGARO

WALEVI kutoka kijiji cha Ngoingwa wamekaribishwa kanisani ili wamjue Mwenyezi Mungu.

Askofu Julius Kamau, wa kanisa la ACK St Stephen, Ngoingwa, Thika, alisema kwa muda mrefu walevi huwa hawamo miongoni mwa Wakristo ambao huhudhuria kanisa ili kupata baraka.

Askofu huyo alisema ni hivi majuzi alipohudhuria mazishi ya mmoja wa jamaa zake na kusikitika jinsi walevi kadha walivyokosa nidhamu.

Alisema alifanya kikao kikubwa nao ili kujadiliana kuhusu masaibu yao.

Baada ya kujadiliana na walevi hao kwa kirefu walevi hao wapatao 30 walihudhuria ibada katika kanisa la ACK St Stephen lililoko katika mtaa wa Ngoingwa, Thika, ili kupata neno la Mungu.

Walevi hao waliohudhuria kanisa walikaribishwa na Askofu Kamau huku wakionyesha furaha yao kwa maombi.

Baadhi ya walevi waliohudhuria kanisa walikaribishwa na Askofu Kamau huku wakionyesha furaha yao kwa maombi. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Askofu Kamau alitoa ushauri kwa wachungaji wote popote walipo wafanye juhudi kuona ya kwamba walevi wanakaribishwa maabadini.

“Mimi kama mchungaji wa ACK Thika, ninatoa wito kwa wachungaji wawape nafasi walevi ili wajue neno la Mungu badala ya kuwadunisha,” alieleza Askofu Kamau.

Alisema walevi hao walifika kanisani wakiwa nadhifu na kuwapongeza kwa kuitikia wito wa kuhudhuria maombi.

Mmoja wa walevi hao ambaye hakutaka Taifa Leo itaje jina lake, alimpongeza Askofu Kamau kwa kuonyesha upendo wake kwao kama walevi.

“Sisi ambao tunatajwa kama walevi tuna matumaini ya kwamba tutazidi kukaribishwa kila mara ili kumuabudu Mungu,” alisema mlevi huyo.

Waumini waliohudhuria ibada hiyo walipongeza juhudi za Askofu Kamau za kuwaleta walevi hao katika njia ya kula chakula cha kiroho.

  • Tags

You can share this post!

Wamalwa aapa kubeba Homeboyz Prinsloo 7s

Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee...

T L