• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Baadhi ya Waislamu Lamu wasikitika kafyu itatatiza tena ibada Mwezi wa Ramadhan

Baadhi ya Waislamu Lamu wasikitika kafyu itatatiza tena ibada Mwezi wa Ramadhan

Na KALUME KAZUNGU

BAADHI ya viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu, Kaunti ya Lamu wana wasiwasi kwamba hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuongeza amri ya kutotoka nje usiku kwa siku 60 zaidi itaathiri pakubwa shughuli za ibada Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Mfungo unatarajiwa kuanza Aprili 13, 2021.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Muungano wa Baraza la Viongozi wa Dini, Ukanda wa Pwani (CICC), Mohamed Abdulkadir, walisema matarajio yao yalikuwa kwamba kafyu ingeondolewa, hasa kwenye eneo la Ukanda wa Pwani ambapo idadi kubwa ya wakazi ni Waislamu.

Bw Abdulkadir alisema kuwepo kwa kafyu wakati wa Ramadhan si jambo linalofaa kwani kutasababisha wengi wa waumini kukosa kufika misikitini kuswali kwa kuhofia kushambuliwa na walinda usalama.

“Sijaridhishwa na Rais wetu Uhuru Kenyatta kuongeza kafyu kwa siku 60. Nilitarajia kuwa kwa vile Mwezi Mtukufu wa Ramadhan umewadia, angetupilia mbali kafyu au hata kufanyia mabadiliko muda wa saa ya kafyu hiyo. Tunahofia kusumbuliwa na polisi wakati tukiingia msikitini kusali wakati wa kafyu,” akasema Bw Abdulkadir.

Ustadh Mohamed Mahfudh alisema ombi lake ni kwamba serikali iwatambue na kuwaruhusu waislamu kusali usiku misikitini bila kizuizi cha kuwepo kwa kafyu wakati wa Ramadhan.

“Kwa sababu kafyu haikuondolewa, ningeomba serikali ifikirie kuwapa ruhusa waislamu kuingia misikitini kusali usiku kila wakati bila kizuizi,” akasema Bw Mahfudh.

Viongozi na waumini hao aidha walimpongeza Rais Kenyatta kwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na makongamano yoyote makubwa ya kijamii nchini.

Ali Shukri alisema maambukizi mengi ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini yamekuwa yakisababishwa na wanasiasa wanaoandaa mikutano bila kuzingatia masharti yaliyowekwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

“Tumefurahia kupigwa marufuku kwa mikutano ya kisiasa nchini. Hilo lilifaa. Hii ya kafyu kuongezwa muda tu ndiyo imetuvunja moyo,” akasema Bw Shukri.

You can share this post!

BETWAY CUP: Congo Boys yataka mechi dhidi ya Gor Mahia iwe...

Vipusa wa Manchester City wapewa Barcelona huku wa Chelsea...