• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
BETWAY CUP: Congo Boys yataka mechi dhidi ya Gor Mahia iwe uwanjani Serani Sports

BETWAY CUP: Congo Boys yataka mechi dhidi ya Gor Mahia iwe uwanjani Serani Sports

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

CONGO Boys FC imesema kwa kuwa wao ni timu ya nyumbani kwa pambano lao la raundi ya timu 64 la Betway Cup dhidi ya Gor Mahia FC, wanastahili kukaribisha wageni katika uwanja wao wa Serani Sports na wala si Mbaraki Sports Club kama ilivyopangwa.

Naibu Kocha wa Congo Boys FC, Omar Faraj amesema wana haki ya mchezo huo kufanyika uwanja wa Serani kwani ndio uwanja wao ambao ni mzuri na unaoweza kuchezewa mechi zozote.

“Hatuoni sababu ya mchuano huo kufanyika Mbaraki Sports Club kwani uwanja wetu unatumiwa kwa mechi kubwa zikiwemo zetu za Ligi ya Taifa Daraja la kwanza na hata zile za Supaligi ya Taifa zinazohusisha timu ya Modern Coast Rangers FC,” akasema Faraj.

Mkufunzi huyo amesema mashindano hayo ya Betway Cup ni sawa na yale ya FA Cup yanayochezwa Uingereza ambapo hata timu zisizokuwa za ligi yoyote zinashiriki na viwanja vyao kutumiwa na huwa ni sifa kubwa kwa timu hizo kucheza dhidi ya timu zenye majina makubwa.

Naibu kocha wa Congo Boys FC, Omar Faraj. Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Kwa timu yetu tumefurahi kupata fursa ya kukutana na timu bora zaidi hapa nchini na tutafurahika zaidi tukicheza mechi hiyo kwenye uwanja wetu wenyewe ambao hauna ubaya wowote,” akasema.

Faraj amesema wanataka kuandikisha historia kuwa walicheza na Gor uwanjani mwao na akaitaka FKF ibadilishe ratiba na kuiweka mechi hiyo uwanja wao na kusema kutoweka mechi hiyo uwanja wao ni sawa na kuwa timu zote mbili zitacheza uwanja wa ugenini.

“Yataka ikubukwe kuwa uwanja tunaoutumia tumeufanyia ukarabati wa hali ya juu kwani hapo zamani ulikuwa ukitumiwa na klabu iliyokuwa maarufu hapa Pwani ya Mwenge (Liverpool),” akasema.

Amesema wamejitayarisha vya kutosha kukabiliana na Gor na wakataka wapewe haki yao ya kucheza mechi yao hiyo ya nyumbani katika uwanja wao. Mechi hiyo imeratibiwa Machi 28, 2021.

You can share this post!

Wanaofariki kuzikwa chini ya saa 72

Baadhi ya Waislamu Lamu wasikitika kafyu itatatiza tena...