• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:48 AM
BBI: Serikali yaandaa rufaa ya uamuzi

BBI: Serikali yaandaa rufaa ya uamuzi

Na RICHARD MUNGUTI

MWANASHERIA Mkuu Kihara Kariuki, Jumanne aliondoa ombi alilowasilisha katika Mahakama Kuu la kusitisha uamuzi wa kufutilia mbali mchakato wa BBI.

Bw Kariuki alisema sasa atapeleka moja kwa moja ombi hilo katika Mahakama ya Rufaa.

“Mahakama ya Rufaa iko na mamlaka na uwezo ya kufutilia mbali uamuzi wa majaji watano waliozima mchakato wa BBI,” alisema Bw Kihara kwenye arifa iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu.

Bw Kariuki alikuwa amewasilisha ombi la awali mnamo Mei 14, siku moja baada ya majaji watano wa Mahakama Kuu kuharamisha BBI.

Katika kesi aliyowasilisha katika mahakama ya rufaa, Bw Kariuki amesema endapo uamuzi wa majaji hao watano utatekelezwa, serikali na wananchi watapata hasara kubwa ikitiliwa maanani rasilmali zilizotumika kufikia sasa.

Aliondoa ombi hilo masaa manne baada ya majaji watano kutoa arifa kwamba wataisikiza ombi lake na kutoa uamuzi wao kufikia Mei 26, 2021.

Majaji hao watano walikuwa wametoa utaratibu wa kusikizwa kwa ombi hilo la Mwanasheria Mkuu na IEBC la kusitisha uamuzi wao.

Majaji Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Enoch Chacha Mwita na Teresia Mumbua Matheka walitoa uamuzi huo uliotia tumbo joto vigogo wa kisiasa nchini mnamo Mei 13, 2021.

Uamuzi huo umezua hisia kali huku wanasiasa wakiwakashifu majaji hao watano kwa kuvuruga mchakato wa kugeuza Katiba.

Lakini chama cha Majaji na Mahakimu (KMJA) kiliwatetea majaji hao kikisema walitoa uamuzi wao kwa mujibu wa sheria.

Katika taarifa kwa wanahabari Katibu mkuu wa KMJA, Derick Kuto alisema shutuma dhidi ya majaji hao watano hazifai kamwe.

You can share this post!

Maafisa wa KDF wahofiwa kuuawa kwa bomu Lamu

KFS yapinga kesi ya kuzima Mpesa Likoni