• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Bei ya mafuta: Kioni asisitiza wabunge ndio wa kulaumiwa

Bei ya mafuta: Kioni asisitiza wabunge ndio wa kulaumiwa

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Ndaragwa Jeremiah Kioni amesema wabunge ndio wenye suluhu ya ongezeko la mara kwa mara la bei ya mafuta ya petroli nchini.

Bw Kioni amesema wanapaswa kuibuka na sheria itakayozuia mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo ambayo ongezeko lake husababisha gharama ya maisha kupanda.

Kulingana na mbunge huyu, mwaka wa 2018 bunge ndilo lilipitisha mswada wa fedha unaoiruhusu Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi Nchini (Epra) kuwa ikitathmini bei ya mafuta ya petroli tarehe 13 na 14 kila mwezi.

“Sisi wabunge ndio tulipitisha sheria hiyo, ambayo inaruhusu Epra kuongeza au kupunguza bei ya petroli. Tuwache kulaumiana kwa msingi wa siasa potovu,” Bw Kioni akasema, akionya kwamba bei itaendelea kuwa ghali hivi karibuni.

“Tarehe 13 na 14 kila mwezi, bei ya mafuta ya petroli nchini lazima itathmniwe, kulingana na msukumo wa bei ya uzalishaji,” akasema.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu, Kioni alisema wabunge wanapaswa kuibuka na mswada wa kubadilisha sheria ya mafuta.

“Tukishaujadili na kupitisha, Rais atatia saini,” akasema, akielezea kushangazwa kwake na baadhi ya wabunge aliosema “wanajifanya kulia machozi ya mamba na raia ilhali wao ndio kiini cha mfumuko wa bei”.

Juma lililopita, Mamlaka ya Kusimamia Sekta za Kawi na Mafuta (Epra) ilitangaza ongezeko la Sh7.58 kwa petroli, mafuta ya dizeli na ya taa yakipanda kwa Sh7.94 na Sh12.97 mtawalia.

Kufuatia mwongozo huo, petroli sasa inauzwa Sh134.72 kwa lita jijini Nairobi na viunga yake.

Lita moja ya dizeli jijini inagharimu Sh107.66 na mafuta taa ambayo hutegemewa na Wakenya wenye mapato ya chini yakiuzwa kwa Sh110.82 kila lita.

Hayo yakijiri, seneti imetishia kuwatimua ofisini mawaziri Charles Keter (Kawi) na John Munyes (Madini na Petroli) baada ya kudinda kuhudhuria kikao kilichoandaliwa na maseneta Jumanne, kuelezea sababu za bei ya mafuta kuongezwa kiholela.

Mfumuko wa bei ya mafuta umechangia gharama ya bidhaa hasa za kula na nauli kuongezeka, mwananchi wa mapato ya chini akilemewa kujiendeleza kimaisha.

You can share this post!

TAHARIRI: Sarakasi hazimfai raia anayeumizwa

Maseneta wapitisha hoja ya ghadhabu dhidi ya mawaziri...