• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Bitok kuchuja kikosi cha Malkia Strikers

Bitok kuchuja kikosi cha Malkia Strikers

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Paul Bitok atapunguza zaidi kikosi chake cha Malkia Strikers hadi kufikia wanavoliboli 12 pekee kufikia mwisho wa mwezi huu.

Hii ni baada ya mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Rwanda kuchuja wachezaji Emmaculate Nekesa wa KCB na Pamela Adhiambo wa Kenya Pipeline kwenye kikosi chake cha wanavoliboli 16 wanaopiga kambi ugani MISC Kasarani.

Kikosi cha mwisho kitakachoteuliwa na Bitok kitaelekea mjini Kurume, Japan mapema mwezi ujao; wiki tatu kabla ya kampeni za Olimpiki kuandaliwa jijini Tokyo, Japan kati ya Julai 23 na Agosti 8.

“Nawashukuru wachezaji hawa wawili ambao wametemwa kwa ukubwa wa mchango wao kikosini. Wamejituma kwa upekee zaidi licha umri wao mdogo wa chini ya miaka 20. Sina shaka kwamba watakuwa kati ya wanavoliboli tegemeo la Malkia Strikers katika kipindi kifupi kijacho,” akasema Bitok.

Aliongeza kuwa hatashawishika kumdumisha yeyote kikosini kutokana na “umaarufu wa jina la mchezaji”.Bitok alifanyia kikosi chake cha wanavoliboli 20 mchujo wa kwanza mnamo Aprili na akawatema Joan Chelagat (Kenya Prisons), Carolyne Sirengo (KCB) pamoja na Josephine Wafula na Jemimah Siangu wa DCI.

Malkia Strikers ambao ni mabingwa mara tisa barani Afrika, wametiwa katika zizi gumu la Kundi A pamoja na Serbia, Jamhuri ya Dominican, Jamhuri ya Korea, Brazil na wenyeji Brazil kwenye Olimpiki.Licha ya kupangwa pamoja na miamba hao kwenye ‘kundi hilo la kifo’, nahodha Mercy Moim, ameshikilia kwamba hakuna kitakachowazuia kutamba jijini Tokyo.

Nyota huyo wa KCB, amefichua kwamba malengo yao ni kuweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza kutoka bara la Afrika kuwahi kutinga nusu-fainali za voliboli kwenye Olimpiki.

Ushindi wowote utakaosajiliwa na Malkia Strikers kwenye Kundi A, utawatosa ndani ya mduara wa 16-bora duniani. Kwa mujibu wa msimamo wa orodha ya viwango bora vya voliboli kimataifa, Kenya kwa sasa inakamata nafasi ya kwanza barani Afrika na inashikilia nafasi ya 23 duniani.

Malkia Strikers watafungua kampeni zao za Olimpiki dhidi ya Japan mnamo Julai 25 kabla ya kupimana ubabe na Serbia, Dominican, Korea na Brazil mtawalia. Itakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kushiriki Olimpiki tangu wongeshe kivumbi cha 2004 jijini Athens, Ugiriki.

Brazil na Japan wamewahi kutwaa medali za dhahabu kwenye Olimpiki mara mbili kila mmoja. Kwa upande wao, Serbia walijizolea medali ya fedha kwenye Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil mnamo 2016 na ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia na bara Ulaya.

“Kampeni za Olimpiki ni tofauti sana na mashindano mengine. Tunaelewa uwezo wa kila mpinzani tutakayekutana naye jijini Tokyo kwa sababu tumezisoma sana video zao kila wanapowajibika uwanjani,” akatanguliza Moim.

“Hata hivyo, tumejifunza mengi katika majukwaa mbalimbali ya voliboli na tutakuwa na kila sababu ya kutawala Kundi A na kuingia nusu-fainali,” akasema kwa kusisitiza kwamba kikosi cha Malkia Strikers kinajivunia mseto mzuri wa chipukizi na wachezaji wazoefu.

Baada ya janga la corona kuvuruga mpango wao wa kupiga kambi ya mazoezi nchini Brazil mwezi huu, Malkia Strikers waliyoyomea jijini Mombasa kabla ya kurejea ugani MISC Kasarani, Nairobi kujifua zaidi.

Kwa upande wake, Bitok ameshikilia kuwa kikosi chake kimeimarika pakubwa japo mazoezi zaidi mjini Kurume yatawapa vinara wa benchi ya kiufundi jukwaa zuri la kutathmini uwezo wa kila mchezaji na kutoa fursa kwa timu nzima kupata uzoefu unaohitajika.

Kikosi cha Malkia Strikers

Noel Murambi, Mercy Moim (nahodha), Leonida Kasaya, Pamela Jepkurui, Sharon Chepchumba, Emmaculate Chemutai, Violet Makuto, Joy Lusenaka, Jane Wacu, Agrippina Kundu, Elizabeth Wanyama, Edith Wisa, Gladys Ekaru, Lorine Chebet.

  • Tags

You can share this post!

Kijana ajeruhiwa baada ya kushambuliwa na kiboko

Barabara kadhaa kufungwa kwa wakati tofauti