• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Daisy: Amepania kutinga upeo wa Gal-Gadot Varsano

Daisy: Amepania kutinga upeo wa Gal-Gadot Varsano

Na JOHN KIMWERE 
TASNIA ya filamu hapa nchini inazidi kufurika wasanii wanaokuja kila kuchao. Daisy Waigumo Karuiru ni kati ya wana dada wanaopania kutinga hadhi ya wana maigizo wa kimataifa miaka ijayo.
”Ingawa tangia nikiwa mtoto nilidhamiria kuhitimu kuwa rubani nilifanikiwa kuhitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya uigizaji kwenye Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU),” amesema na kuongeza kuwa ameshiriki uigizaji kwa miaka saba.
Alivutiwa na uigizaji baada ya kutazama filamu ya mwigizaji wa Nollywood, Mercy Johnson Okojie iitwayo Dumebi the Dirty Girl. Kisura huyu  anasema mwaka 2013 aliota akishiriki uigizaji na waigizaji mahiri aliokuwa akiwatazama kwenye runinga.
Katika mpango mzima binti huyu aliyezaliwa mwaka 1995 amepania kutinga upeo wa mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Israel, Gal Gadot-Varsano ambaye anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Wonder Woman.’ Binti huyo kwa sasa amezamia uigizaji pekee baada ya kuacha ualimu katika shule ya msingi.

 
MAFUNDI
Dada huyu ameshiriki uigizaji na makundi mawili ‘Nation players Theatre ‘na ‘Forever Arts Group,’ ambayo hushughuli na michezo ya kuigiza kwa kufuata mwongozo wa vitabu vya riwaya. Hata hivyo anajivunia kushiriki filamu tatu kama mwigizaji wa ziada ambazo zilizopata mpenyo na kuonyeshwa kwenye runinga.
Msanii chipukizi Daisy Waigumo Karuiru…PICHA/JOHN KIMWERE
”Nina fuaraha kwangu najivunia hatua ambayo nimepiga kufikia sasa ambapo nimeshiriki filamu hizo zikiwa ‘Mafundi (NTV), Varshita (Maisha magic East Africa) na My Two Wifes (KTN),” akasema.
Anaponda vyombo vya habari nchini ambazo huwapatia filamu za kigeni kipau mbele badala ya kuonyesha kazi za wazalendo kuwatia moyo kazi zao. Anasema hatua hiyo imechangia Wakenya wengi kuegemea filamu za kigeni kutoka mataifa yaliyopiga hatua katika sekta ya maigizo kama Nigeria, Ghana, Tanzania na Afrika Kusini kati ya mengine.
 
NOLLYWOOD
Anasema kwa waigizaji wa Afrika angependa sana kufanya kazi na wasanii mahiri kama Destiny Etiko na Uche Jombo zawa wa Nigeria. Wawili hao wameshiriki filamu kama ‘The Storm,’ ‘Idemili,’ na ‘Lagos Cougars,’ ‘Mrs Somebody’ mtawalia.
Kwa wasanii wa hapa nchini anaota kujikuta jukwaa moja na wenzie kama Sera Teshna Ndanu na Sarah Hassan. Anasema miaka mitano ijayo amepania kuwa mwigizaji mkubwa Afrika pia kuanzishwa brandi yake ili kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji wanaokuja na kukuza tasnia ya filamu.
”Binafsi sina shaka kutaja kuwa natamani sana kumiliki brandi ya kuzalisha filamu maana ninaendelea kupata maarifa kila kuchao.” Anasema malipo duni pia kukosa ajira ni kati ya changamoto ambazo wengi wao hupitia.
Anashauri wenzie kuwa wabunifu, wajiamini, wajiheshimu pia watie bidii zaidi bila kusahau kumuweka Mungu mbele ili kufikia malengo yao katika tasnia ya maigizo.
  • Tags

You can share this post!

Dammah: Tunahitaji kuwa wabunifu kwenye kazi zetu mwanzo

Kysa Karengata: Corona imevuruga sekta ya spoti pakubwa