• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Kysa Karengata: Corona imevuruga sekta ya spoti pakubwa

Kysa Karengata: Corona imevuruga sekta ya spoti pakubwa

Na JOHN KIMWERE 
MLIPUKO wa virusi vya corona duniani umevuruga sekta ya michezo pakubwa hasa katika mataifa ya Afrika.
Janga la virusi hivyo limechangia timu nyingi za fani mbali mbali kukosa wadhamini baada ya biashara kibao kuadhirika. KYSA Karengata FC ni kati ya vikosi vinavyopitia wakati mgumu kwa kukosa ufadhili muhula huu.
Licha ya hayo klabu hii ni miongoni mwa timu zinazoshiriki mechi za Kundi B kufukuzia ubingwa wa taji la Nairobi West Regional League (NWRL). ”Kiukweli bila ufadhili sio rahisi klabu yoyote kuendeleza shughuli za mchezo wowote.
Muhula huu tumejikuta njiapanda kwani wasamaria wema wamesepa maana virusi vya corona vimechangia wengi kupoteza ajira na kuharibu biashara nyingi,” alisema meneja wake, Joseph Otieno Oloo na kuongeza kuwa ukosefu wa ufadhili umewakosti pakubwa kwenye kampenio zao.
Meneja huyo anatoa wito kwa wahisani wajitokeze na kuzipatia msaada klabu zinazoshiriki soka la kiwango cha mashinani ambazo mara nyingi hukuza wachezaji chipukizi. KYSA Karengata ya kocha, Benson Godia na Kelly Nanjira Ogutu iliyopania kumaliza kati ya nne bora msimu huu imejikuta katika mduara wa timu nne za mwisho zinazokondolea macho kushushwa ngazi.
KARE: Timu ya KYSA Karengata inayoshiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu…PICHA/JOHN KIMWERE
Huku ikiwa imebakisha mechi saba kukamilisha ratiba yake msimu huu, kocha Godia anasema bado hawajavunjika moyo maana wamepania kujituma kiume na kushinda mechi kadhaa ili kujinasua kutoka mduara wa kuteremshwa ngazi.
KYSA inajivunia kati ya wachezaji mahiri kama Elvis Munyao (straika), Mathew Luchacha (beki wa kati), Wisdom Wafula (kiungo) bila kuweka katika kaburi la sahau Mitchell Saya. Timu hii inajivunia kukuza wachezaji wachache akiwamo Darius Gichoi ambaye soka lilimsaidia kupata ufadhili kusafiri nchini Marekani kabla ya kubadili uraia wake.
Pia yupo Maurice Kadilo aliyewahi kupigia Uweza FC ambayo hushiriki kampeni za Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Kadhalika imenoa makucha ya Robert Arasa aliyekuwa kati ya makocha wa Kangemi Allstars ambayo hushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza muhula huu.
KYSA awali ikijulikana kama St Andrews Golden Stars kabla ya kubadili jina hilo mwaka 2011, inajivunia kubeba mataji 18 tangia ianzishwe mwaka 2002. Mataji hayo ni kama Karen Lang’ata Association Cup, Ruth Wakapa Cup,  Ongata Rongai Cup, Sian Group of flowers Nakuru Cup na Parklands Left Foot Senior Cup.
Pia ilibahatika kuwakilisha eneo la Lang’ata kwenye fainali za kipute cha Sakata Ball Safaricom Challenge 2011.
  • Tags

You can share this post!

Daisy: Amepania kutinga upeo wa Gal-Gadot Varsano

Ziara ya Rais eneo la Magharibi yayumba